Ayatullah Khamenei ameashiria ukuaji endelevu na nguvu ya ndani ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kusema: "Kundi
hili hivi sasa limekuwa kituo kikubwa na chenye vifaa kamili na taasisi
kubwa zaidi ya kupambana na ugaidi duniani, ambapo majeshi makubwa
zaidi ulimwenguni hayana uwezo wa kufanya mfano wa yale yanayofanywa na
kundi hili."
Tangu Imam Khomeini (MA) alipotoa amri ya kuanzishwa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu IRGC mnamo Aprili 1979, taasisi hii ya wananchi daima imekuwa mstari wa mbele katika kutetea Mapinduzi, nchi na taifa, na bila shaka ina rekodi nzuri ya utendaji katika uwanja huu.
Utendaji wa Jeshil la Walinzi wa Mapinduzi katika kipindi cha vita vya kujitetea kutakatifu, kuzima njama na fitna hatari za maadui wa mfumo wa Kiislamu, kutekeleza miradi ya ujenzi na utengenezaji silaha za kisasa, ikiwa ni pamoja na makombora na mifumo ya anga za mbali, yote hayo yanaonyesha kuongezeka kila siku mafanikio ya taasisi hii yenye fahari, mafanikio ambayo yamezidisha hasira ya maadui na hivyo kuwafanya waendelee kutoa mashinikizo na kuiwekea vikwazo taasisi hii muhimu ya Mapinduzi ya Kiislamu.Wakati wa vita vya kulazimishwa vya utawala wa Saddam dhidi ya Iran, ambavyo vilianzishwa kwa lengo la kusambaratisha Mapinduzi ya Kiislamu na kuigawa Iran, Walinzi wa Mapinduzi walidhihirisha uwezo wao halisi ambapo walikuwa na nafasi muhimu katika kuyarudisha nyuma majeshi ya Iraq na kushinda njama za maadui.
Baada ya kumalizika vita hivyo, mbali na kutekeleza majukumu yake makuu ambayo ni kulinda mfumo wa Kiislamu, na kwa kuzingatia amri ya Kiongozi Muadhamu, Walinzi wa Mapinduzi waliingia katika uwanja wa ujenzi wa nchi. Kwa msingi huo, IRGC ilichukua jukumu muhimu la kutekeleza miundomsingi na miradi mbalimbali ya mafuta na gesi na vilevile kujenga miundombinu muhimu ya maendeleo katika maeneo ya vijijini ikiwa ni pamoja na barabara, madaraja, shule, makazi na vituo vya afya kwa manufaa ya wakazi wa maeneo hayo.
Ayatullah Khamenei ametathmini utendakazi wa IRGC katika suala la ujenzi na miundombinu kuwa wenye fahari, unaong'ara na wa kipekee katika baadhi ya sekta na kusisitiza: Walinzi wa Mapinduzi wamewahudumia wananchi kwa nguvu zao zote katika huduma za umma, kuondoa umasikini, majanga ya kimaumbile na mabalaa kama corona.
Katika miaka ya hivi karibuni na sambamba na kuongezeka vitisho vya kiutamaduni vya maadui, makabiliano ya IRGC na vitisho laini pia yameongezeka kwa kadiri kwamba hii leo moja ya nguzo muhimu zaidi za IRGC ni idara inayoshughulika na masuala ya kiutamaduni. Idara hii imeweza kuchukua hatua madhubuti za kukabiliana na vitisho na wakati huo huo kukuza masuala ya kiutamaduni katika ngazi ya jamii.
Ni muhimu kukumbusha hapa kuwa miongozo na mapambano ya jeshi la IRGC yameleta amani na usalama sio tu ndani ya nchi bali pia katika mataifa ya Kiislamu ya eneo. Katika miaka ya karibuni, IRGC imeweza kuunda muhimili na muungano wenye nguvu katika mapambano dhidi ya ugaidi katika eneo, hasa nchini Syria.Makamanda wa IRGC, akiwemo Luteni Jenerali Haj Qassem Soleimani, wameweza kuwashinda magaidi na kuyakomboa maeneo yaliyokuwa yametekwa na magaidi hao kwa kuhamasisha uwezo wa ndani na kusaidia kuunda harakati za mapambano kama vile Hashd al-Shaabi nchini Iraq na Wapiganaji wa Ulinzi wa Kitaifa wa Syria.
Ukweli wa mambo ni kwamba nafasi ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu katika kudumisha usalama wa nchi na kupambana vikali na wahalifu na makundi ya kigaidi, na wakati huo huo kukuza uwezo wa kijeshi wa Walinzi wa Mapinduzi, kumezuia uchokozi wa maadui kwa namna ambayo ilikuwa haijawahi kuonekana tena katika historia ya eneo zima la Mashariki ya Kati. Hii ni kusema kuwa maadui hawawezi tena, kama ilivyokuwa kawaida zamani, kufikiria kuanzisha uchokozi wa kijeshi katika eneo.
Katika matamshi yake pia, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kupunguzwa na kutokaririwa tena maneno ya "chaguo la kijeshi liko mezani" kunatokana na uwezo na nguvu ya IRGC ya kuzuia hujuma ya adui na kuongeza: "Kila mtu sasa anajua kuwa maneno haya hayana uzito, maana wala thamani yoyote."
342/