30 Agosti 2023 - 20:08
 Nyufa mpya katika uhusiano wa Saudi na Marekani

Ahmad Kazemzadeh wa gazeti la Financial Times ameandika, akinukuu vyanzo vya habari, kwamba Saudi Arabia, ambayo haikufurahishwa na masharti yaliyotolewa na Marekani kwa ajili ujenzi wa kinu cha nyuklia nchini humo, inachunguza mapendekezo ya China, Russia na Ufaransa ya kujenga kinu cha nyuklia nchini Saudia.

Mohammed bin Salman, mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia, yuko tayari kuanzisha ushirikiano na kampuni inayomilikiwa na serikali ya China kwa ajili ya kufunga mkataba wa kujenza kinu cha nyuklia nchini Saudia iwapo mazungumzo na Marekani yatafeli.

Awali, gazeti la Wall Street Journal, liliwanukuu maafisa wa Saudi Arabia na kuripoti kwamba, Kampuni ya Kitaifa ya Nyuklia ya China inayojulikana kwa jina la "CNNC" imetoa pendekezo kwa Riyadh kujenga kinu cha nyuklia katika mkoa wa mashariki mwa nchi hiyo, karibu na mpaka na Qatar na UAE.

Marekani haiko peke yake katika suala hili, kwani hata utawala wa Kizayuni, ambao umeanzisha jitihada kubwa kwa ajili ya kuanzisha uhusiano rasmi na Saudi Arabia, sasa na baada ya serikali ya Riyadh kutaja suala la kupata nguvu za nyuklia kuwa ndilo sharti la kuanzisha uhusiano na utawala huo ghasibu, kadhia hiyo imeibua hitilafu kubwa ndani ya Israel na hivyo kuzidisha mizozo ndani inayozidi kuitafuna Israel.

Tunaporejea kenye kadhia ya uhusiano wa Marekani na Saudia tunaona kuwa, ushahidi uliopo unaonyesha kwamba, uhusiano huo unazidi kudhoofika siku baada ya siku, na Saudi Arabia inatafuta washirika wapya na mbadala katika kanda ya Mashariki ya Kati na dunia. Gazeti la Telegraph limendika kuhusiana na suala hilo kwamba, sasa baada ya miaka 13, kumekuwa na mabadiliko duniani na miungano mipya inajitokeza kwa kasi. Katika dunia inaozidi kuwa na kambi nyingi, Saudi Arabia inatafuta washirika wengine wa usalama ambao hawasumbuliwi na machafuko na ukosefu wa utulivu wakati wa uchaguzi, au wasioikosoa sana Saudia kuhusu masuala ya haki za binadamu.

Katika kipindi cha miaka 15 iliyopita, utegemezi wa Washington kwa mafuta ya Ghuba ya Uajemi umepungua kwa kiwango kikubwa, na kwa upande mwingine, uzalishaji wa nishati ndani ya Marekani umeongezeka kwa kadiri kwamba, kwa sasa Marekani inaagiza chini ya asilimia sita ya mahitaji ya mafuta yake kutoka Saudi Arabia.

Kwa msingi huo tunaweza kusema kwamba, mlingano wa "mafuta mkabala wa usalama", ambao ulikuwa nguzo muhimu ya uhusiano wa Saudi na Marekani kwa miongo kadhaa, sasa umetoweka na haupo tena.

Mvutano katika uhusiano wa Saudi Arabia na Marekani ulishika kasi pale viongozi wa Saudia walipoamua kupunguza uzalishaji wa mafuta licha ya Ikulu ya White House kuamini kuwa, imekubaliana na Riyadh juu ya kuongeza uzalishaji wa bidhaa hiyo.