12 Oktoba 2023 - 16:24
Katika mazungumzo yao ya kwanza: Rais wa Iran na Mwanamfalme wa Saudia wajadili hali ya Gaza

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudi Arabia wamezungumza kwa njia ya simu kuhusu matukio ya Palestina na ulazima wa kusitishwa jinai za kivita zinazofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Mohammed Jamshidi, Mkurugenzi wa Masuala ya Siasa wa Ofisi ya Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ameandika katika mtandao wa kijamii wa X, kwamba, mazungumzo kati ya Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Sayyid Ebrahim Raisi na Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Saudi Arabia, Muhammad bin Salman, yamejadili haja ya kukomesha jinai za kivita na kwamba pande zote mbili zimetilia mkazo umoja wa Ulimwengu wa Kiislamu zikisisitiza kuwa jinai zinazofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel na taa ya kijani na baraka za Marekani kwa jinai hizo ndiyo sababu ya ukosefu wa usalama na uharibifu mkubwa kwa utawala huo na waungaji mkono wake.Wakati huo huo televisheni ya Aljazeera ya Qatar imelinukuu Shirika la Habari la Serikali la Saudi (SPA) , kwamba Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa nchi hiyo, Muhammad bin Salman amesisitiza msimamo wa nchi hiyo wa kupinga mashambulizi yanayowalenga raia, na ulazima wa kuheshimiwa kanuni za sheria za kimataifa za kibinadamu, akielezea wasiwasi wake mkubwa kuhusu hali ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza na madhara yake kwa raia wa eneo hilo. Aljazeera imeripoti kuwa, hii ni mara ya kwanza kwa viongozi hao wawili kufanya mazungumzo ya simu tangu baada ya mapatano ya kurejesha uhusiano baina ya Tehran na Riyadh yaliyosimamiwa na China mwezi Machi mwaka huu.

342/