Radiamali ya Iran inatolewa baada ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki ukiwa chini ya mashinikizo ya madola ya Magharibi, kupitisha azimio la kisiasa na lisilo la kiutaalamu dhidi ya miradi ya amani ya nyuklia wa Iran.
Azimio lililowasilishwa mbele ya Bodi ya Magavana ya IAEA na nchi tatu za Ulaya za Uingereza, Ufaransa na Ujerumani dhidi ya Iran, lilipasishwa Jumatano ya tarehe 5 Juni kwa kura 20 za ndio na 12 za hapana na cha ajabu halikuashiria hata kidogo ushirikiano mzuri ambao Iran imekuwa ikiuonesha kwa IAEA tena kwa kukiri hivyo mara chungu nzima wakala huo.
Hii ni mara ya kwanza baada ya miezi 18 kwa Bodi ya Magavana ya wakala huo kuchukua uamuzi wa aina hiyo dhidi ya Iran. Baada ya makubaliano ya nyuklia yanayojulikana kwa jina la JCPOA, azimio la kwanza dhidi ya Iran lilitolewa na Bodi ya Magavana wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki mwezi Juni 2022, na nchi za Magharibi zilieleza kutoridhishwa kwao na ushirikiano wa Iran kwa wakala huo. Azimio hili lilipigiwa kura na Baraza la Magavana kwa pendekezo la Marekani, Uingereza, Ujerumani na Ufaransa na kisha likaidhinishwa. Azimio la pili la Baraza la Magavana kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran baada ya mapatano ya JCPOA pia lilitolewa mwezi Novemba mwaka huo huo huo wa 2022. Mara hiyo pia, azimio lililopendekezwa na Marekani na Troika ya Ulaya lilipasishwa.
Ingawa baada ya azimio hili, kauli kadhaa zilitolewa na madola hayo dhidi ya Iran, lakini katika kipindi chote hiki hakukutolewa tena azimio jipya dhidi ya Iran hadi hili la Jumatano iliyopita. Lugha iliyotumika katika azimio la juzi ni sawa na ile iliyotumika katika maazimio mawili yaliyotangulia ambapo mara hii pia eti Iran imetakiwa kupanua mara moja ushirikiano wake na IAEA na kuwaruhusu wakaguzi wa taasisi hiyo ya kimataifa kutekeleza majukumu yao ya kufuatilia na kukagua shughuli za nyuklia za Iran.
Azimio hili limekabiliwa na radiamali ya Jamhuri ya Kiiislamu ya Iran. Uwakilishi wa Iran katika asasi za kimataifa umetangaza kuwa, hadi sasa Tehran imetoa ushirikiano kamili kwa wakala wa IAEA na shughuli zote za miradi ya nyuklia ya Iran zimekuwa zikifanyika chini ya usimamizi kamili wa wakala huo. Iran imeeleza bayana kwamba, chimbuko la tuhuma dhidi ya Iran ni upande wa tatu wenye nia mbaya ambao ni utawala haramu wa Israel.
Ali Bagheri Kani, Kaimu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alisema katika kikao cha Baraza la Mawaziri siku ya Jumatano kwamba: Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomi (IAEA) ni taasisi ya kiufundi na inatarajiwa kuyaona mataifa yakiwemo wanachama wa Bodi ya Magavana ya wakala huo yakiwa na mienendo ya kiufundi.
Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imelaani vikali hatua ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki, IAEA, ya kupitisha azimio dhidi ya Iran, na kusisitiza kwamba hatua hiyo haitaweza kudhoofisha mipango yake ya maendeleo ya nyuklia.
Taarifa hiyo imesema: "Kupitishwa kwa azimio hilo hakutaathiri azma ya Jamhuri ya Kiislamu ya kuendelea na matumizi yake ya amani ya nishati ya nyuklia na kutekeleza mipango yake ya maendeleo ya nyuklia kulingana na haki zinazotolewa kwa nchi chini ya makubaliano ya kimataifa."
Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran imetaja hatua hiyo ya IAEA kuwa ni ya kisiasa na isiyo na manufaa" na ni njama za baadhi ya nchi za Magharibi za kutumia vibaya mifumo ya kimataifa kulenga na kuziandama nchi huru.
Kwa upande wake, msemaji wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran amesema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu kamwe haitofumbia macho haki zake za nyuklia na itasimama imara kulinda na kutetea haki zake hizo.
Behrouz Kamalvandi amesema Jamhuri ya Kiislamu itakabiliana vilivyo na azimio hilo la kisiasa la IAEA na itachukua hatua za kivitendo za kupambana na mashinikizo hayo mapya ya madola ya Magharibi.
Hatua ya IAEA dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imechukuliwa katika hali ambayo, Rafael Grossi, Mkurugenzi Mkuu wa wakala huo hadi sasa ameonekana kutoa matamshi yaliyo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambayo kimsingi yana utashi wa kisiasa na ambayo yanakwenda sambamba na siasa za kidhalimu za Marekani.
Kwa kuzingatia hayo, hatua ya sasa na kupitishwa kwa azimio dhidi ya Iran wakati Tehran iko katika harakati za kufanya uchaguzi wa mapema wa rais, ni mtazamo wa kisiasa ambao utaathiri uhusiano kati ya Tehran na wakala huo. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imethibitisha mara nyingi kwamba, katu haitakaa katika meza ya mazungumzo kwa sababu ya mashinikizo ya kigeni na kamwe haiko tayari kulegeza kamba au kuufumbia macho haki na maslahi yake.
342/