Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Ahlul-Bayt (a.s) -ABNA- Muqtada al-Sadr, kiongozi wa harakati ya Sadr nchini Iraq, leo Jumatano, kupitia ujumbe kwenye mtandao wa kijamii X (zamani Twitter), ametahadharisha kuwa mgogoro wa kimataifa wa maji sasa umeikumba Iraq, na kengele ya hatari tayari imelia.
Al-Sadr alieleza kuwa kupungua kwa kasi kwa vyanzo vya maji nchini Iraq – ikiwemo kupungua kwa akiba ya ndani ya maji, ukosefu wa mvua, na kupungua kwa kiwango cha maji katika mito – ni hali inayohitaji hatua za haraka kutoka kwa taasisi husika.
Ametoa wito wa kuanzishwa kwa mazungumzo na nchi jirani ya Uturuki, kwa lengo la kuongeza mgao wa maji kwa Iraq, na wakati huohuo kusisitiza haja ya kuchukua hatua za ndani, zikiwemo:
1- Ujenzi wa mabwawa na hifadhi za maji.
2- Adhabu kwa wanaotumia vibaya vyanzo vya maji.
3- Uondoaji wa chumvi kutoka kwenye maji ya bahari (maji chumvi).
4- Matumizi ya visima kwa ajili ya umwagiliaji wa mazao ya kilimo.
Kiongozi huyo wa kisiasa alionya kuwa ucheleweshaji wowote katika kushughulikia mgogoro huu wa maji utaleta athari kubwa katika sekta ya afya, kilimo, na maeneo mengine ya maisha. Akasema kuwa wananchi wa Iraq, ambao tayari waliteseka kutokana na mgogoro wa umeme, sasa wako hatarini kuathiriwa na uhaba wa maji.
Your Comment