
Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Kuadhimisha kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Amirul-Mu’minin Imam Ali bin Abi Talib (a.s.) lilifanyika jana katika Madrasa ya Imam Ali (a.s.) iliyopo Vikindu, likiwa katika hali ya kiroho na furaha ya kiimani, kwa ushiriki wa wanazuoni, wanafunzi wa elimu ya dini, viongozi wa kijamii pamoja na wapenzi wa Ahlul-Bayt (a.s.).
Baraza la Maulid lilianza kwa kisomo kitukufu cha Aya za Qur’ani Tukufu, kikifuatiwa na maneno ya utangulizi yaliyobainisha umuhimu wa tukio hili tukufu na nafasi ya pekee ya Imam Ali (a.s.) katika Uislamu, kama mfano wa haki, ucha-Mungu, ushujaa na elimu.
Katika ratiba ya baraza hilo, zilitolewa hotuba na mawaidha mbalimbali yaliyogusia maisha na mwenendo wa Imam Ali (a.s.), yakisisitiza nafasi yake katika kuutetea Uislamu na mchango wake mkubwa katika kujenga jamii yenye misingi ya uadilifu, huruma na kutetea wanyonge.
Aidha, wahadhiri walieleza mafunzo ya kimaadili na kijamii yanayopatikana kupitia sera na tabia zake, hususan katika uongozi na mahusiano ya kijamii.
Baraza pia lilipambwa kwa qaswida na mashairi ya kumsifu Imam Ali (a.s.), yaliyoonyesha furaha na mapenzi ya waumini kwa Ahlul-Bayt (a.s.), huku washiriki wakionesha hisia za shukrani na mshikamano katika kuadhimisha tukio hilo adhimu.
Mwisho wa baraza, washiriki waliinua mikono yao kwa dua, wakimuomba Mwenyezi Mungu ailinde Umma wa Kiislamu, awape waumini taufiki ya kufuata mafundisho na mwenendo wa Imam Ali (a.s.), na ayajaalie majlisi kama haya yaendelee kuwa chanzo cha elimu, mwamko wa kiroho na maadili mema katika jamii.

Your Comment