15 Septemba 2025 - 23:41
Source: Parstoday
Al Mayadeen: Rasimu ya taarifa ya kikao cha Doha itakuwa ya kurudia kuulaani tu utawala wa kizayuni

Rasimu ya mkutano wa dharura wa wakuu wa nchi za Kiarabu na Kiislamu unaofanyika katika mji mkuu wa Qatar, Doha inaonyesha kuwa, taarifa itakayotolewa mwishoni mwa kikao hicho itakuwa ni ya kulaani tu vitendo vya utawala wa kizayuni wa Israel.

Mkutano wa dharura wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu, OIC na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu umepangwa kufanyika leo Jumatatu katika mji mkuu wa Qatar, lengo likiwa ni kujadili hatua za kuchukua dhidi ya shambulio la juma lililopita lililofanywa na utawala haramu wa Israel mjini Doha, huku ikitarajiwa kwamba mara hii nchi za Kiislamu zitachukua msimamo tofauti.

Hata hivyo, kwa mujibu wa chaneli ya televishehni ya Al-Mayadeen, sehemu kuu za rasimu ya taarifa itakayotolewa mwishoni mwa mkutano huo zimeonyesha kuwa kisitarajiwe kitu kingine zaidi ya tamko la kulaani tu.

Katika taarifa hiyo, mashambulizi ya hivi majuzi dhidi ya Qatar yanaelezwa kuwa ni kitendo kinachohatarisha uthabiti wa kikanda na kizuizi kikubwa kwa juhudi za kusitisha vita huko Ghaza.

Huku ikiashiria jinai za mauaji ya kimbari na maangamizi ya kizazi katika Ukanda wa Ghaza na kuendelezwa ujenzi wa vitongoji vya walowezi katika Ukingo wa Magharibi, taarifa hiyo imelaani vitendo hivyo na kuonya kwamba hujuma hizo za Wazayuni zinatishia kufuta mafanikio yote ya hatua za kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala ghasibu wa Israel.

Taarifa hiyo imesisitiza pia kuunga mkono mipango ya upatanishi ya Qatar, Misri na Marekani ili kukomesha uchokozi na kurejesha amani huko Ghaza. Aidha, imetoa indhari juu ya matokeo hasi ya jaribio lolote la kulazimisha ukweli mwingine mpya katika eneo na kutekeleza maamuzi yanayoweza kupelekea kunyakuliwa maeneo zaidi ya ardhi za Palestina.

Taarifa ya mwisho ya mkutano huo inasema, amani ya kudumu katika Mashariki ya Kati itapatikana pale tu zitakapopatikana haki kamili za watu wa Palestina na kutekelezwa Mpango wa Amani wa Waarabu ukiwa ndio msingi mkuu wa kufikia lengo hilo.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, makundi ya Muqawama ya Palestina yalieleza katika ujumbe yaliotoa siku ya Jumapili: "wajibu wenu wa kihistoria na wa kibinadamu unakutakeni muchukue misimamo thabiti dhidi ya jinai ya utawala wa Kizayuni ambayo itakwenda mbali zaidi ya kutoa taarifa tu na kufikia kiwango cha uchukuaji hatua za kivitendo na za pamoja".

Makundi ya Palestina yametaka pia kutekelezwa mkataba wa pamoja, kutumia silaha ya mafuta, kuwekwa vikwazo vya pande zote vya Waarabu dhidi ya utawala wa Kizayuni, na kuchukuliwa hatua za haraka sana kwa kushirikiana na Jamii ya Kimataifa ili kuuwekea vikwazo utawala huo.../

Your Comment

You are replying to: .
captcha