15 Septemba 2025 - 23:42
Source: Parstoday
Waziri wa Ulinzi wa Venezuela aonya askari wa US: Msiwe wapumbavu

Waziri wa Ulinzi wa Venezuela, Vladimir Padrino López amelaani kitendo cha Marekani cha kupeleka vikosi vyake vya majini kwenye visiwa vya Caribbean kwa kisingizio kupambana na ulanguzi wa dawa za kulevya, akisisitiza kuwa lengo halisi la Washington ni kuangusha serikali halali ya Rais Nicolas Maduro.

Akiwahutubu moja kwa moja wanajeshi wa Marekani, Padrino López ametilia shaka heshima na madhumuni ya operesheni hiyo na kusema: "Msiharibu heshima zenu za kijeshi. Je, mnajitoa muhanga kwa operesheni hiyo ya aibu? Je, hamfikiri kwamba mnakiuka uadilifu wenu wa kijeshi?"

Waziri wa Ulinzi wa Venezuela amewaonya askari wa Marekani, na kuwataka watu wenye busara badala ya kuburuzwa kwenyen maamuzi ya kipumbavu

Mvutano kati ya Marekani na Venezuela unazidi kuongezeka huku utawala wa Donald Trump ukizidisha kampeni yake ya mashinikizo, kwa kutumia madai ya vita dhidi ya mihadarati kuhalalisha vitendo vya tarajiwa vya kijeshi dhidi ya serikali huru ya Caracas.

Hivi kribuni, Rais wa Venezuela, Nicolas Maduro alisema kuongezeka uwepo wa majeshi ya Marekani katika eneo la Caribbean kunalenga kuipindua serikali yake, na kusisitiza kuwa yuko tayari "kutangaza jamhuri yenye silaha" ikiwa nchi hiyo itashambuliwa na wanajeshi hao wavamizi.

Ameonya kwamba, nchi yake itagura kutoka kwenye 'siasa' na kuingia kwenye "mapambano ya kutumia silaha" iwapo Marekani itaanzisha mashambulizi ya kijeshi dhidi ya taifa hilo. Hii ni baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump kutishia kuzitungua ndege za kijeshi za Venezuela iwapo 'zitakuwa hatari' kwa majeshi ya Marekani.

Marekani na Venezuela zimekuwa katika uhasama na misiguano kwa muda mrefu, huku Washington ikiunga mkono viongozi wa upinzani na kuweka vikwazo shadidi vinavyolenga kuisakama serikali ya Maduro.

Your Comment

You are replying to: .
captcha