15 Septemba 2025 - 23:43
Source: ABNA
Kwa nini maandamano ya kupinga kuungwa mkono Israel yameongezeka barani Ulaya?

Maelfu ya watu wamemiminika barabarani mjini Berlin kupinga sera za Ujerumani katika eneo la Asia Magharibi hususan za kuunga mkono jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel.

Takriban raia 15,000 wa Ujerumani walikusanyika Brandenburg mjini Berlin, wakiwa wamenyanyua juu bendera za Palestina, na kutangaza upinzani wao dhidi ya sera za Berlin katika eneo la Asia Magharibi. Waandamanaji huku wakipiga nara kama vile "Sitisha mauaji ya halaiki huko Gaza," wameitaka serikali ya Ujerumani kuongeza juhudi za kidiplomasia ili kumaliza vita huko Ghaza.

Katika miezi ya hivi karibuni mashinikizo la umma kwenye nchi za Ulaya hususan Ujerumani dhidi ya sera za madola ya Ulaya za kuunga mkono jinai za Israel yameongezeka sana. Moja ya matakwa makuu ya waandamanaji ni kusitishwa uungaji mkono wa kijeshi kwa Israel na kukomeshwa kushehenezwa silaha utawala katili wa Tel Aviv.

Hii ndio maana, maoni ya umma katika nchi mbalimbali za Ulaya yamezidi kukasirishwa na uungaji mkono wa kijeshi wa nchi zao kwa Israel hasa baada ya kutokea mashambulizi makubwa ya Israel dhidi ya Ghaza, mwezi Oktoba 2023, ambayo yalisababisha vifo na kujeruhi maelfu ya Wapalestina.

Maandamano hayo yanaakisi mwelekeo unaozidi kukua wa kushinikiza kukomeshwa uungaji mkono wa kijeshi kwa Israel, na suala hilo linatoa mashinikizo kwa utawala wa Kizayuni wa kukomesha mauaji ya umati huko Ghaza, na kuzidi kuleta mabadiliko katika sera za kigeni za nchi za Ulaya.

Raia wengi wa Ulaya sasa si tu hawaridhishwi na kuendelea vita na uharibifu wa Ghaza, lakini pia wamechoshwa na sera za viongozi wa Ulaya za kuunga mkono kibubusa utawala katili wa Israel. Wengi wao wanachukulia uungaji mkono wa Ulaya kwa Israel na kushehenezwa silaha utawala huo dhalimu kuwa ni kushiriki moja kwa moja nchi za Ulaya katika jinai zinazoendelea kufanywa na Tel Aviv dhidi ya Wapalestina hususan wa Ukanda wa Ghaza. Wananchi wa Ulaya hawawezi tena kuona fedha zao za kodi zinatumiwa na baadhi ya wanasiasa kushiriki katika mauaji ya kimbari ya Ghaza. Hasa kwa kutilia maanani kwamba maandamano hayo, ambayo awali yalikuwa yanafanyika kwa idadi ndogo katika nchi mbalimbali za Ulaya, sasa yamekuwa yakifanyika kwa idadi kubwa ya watu kiasi kwamba sasa yanaweza kuathiri maamuzi ya serikali za Ulaya.

Ushahidi wa hayo ni kwamba katika miezi ya hivi karibuni, baadhi ya nchi za Umoja wa Ulaya zimeamua kuchukua hatua ya kuitambua Palestina kuwa taifa huru kutokana na mashinikizo ya maandamano hayo. Kitendo hicho kinaonyesha kuweko tofauti baina ya sera za zamani za nchi hizo ambazo mara kwa mara zilikuwa zinaunga mkono kibubusa jinai zote za Israel. Kutambuliwa kuundwa taifa la Palestina katika kikao cha mwisho cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwa uungaji mkono wa nchi 142 kunaweza kutathminiwa kuwa ni sehemu ya athari za maandamano hayo makubwa ya kuliunga mkono taifa la Palestina, barani Ulaya.

Matukio haya yanaonekana waziwazi hasa katika kuigomea Israel na kusitisha kuupa silaha utawala wa Kizayuni. Mashirika mengi ya kutetea haki za binadamu na wanaharakati wa masuala ya kijamii barani Ulaya wanatoa mwito wa kuwekewa vikwazo vingi Israel, hasa kusitisha uuzaji wa silaha kwa Tel Aviv. Baadhi ya nchi za Ulaya hivi sasa zinapita kwenye mabadiliko yanayozidi kuongezeka katika suala hili kiasi kwamba, maafisa wa ngazi za juu wa Ulaya wamezungumzia uwezekano wa kupitia upya uhusiano wao wa kijeshi na Israel. Hii ni kweli hasa baada ya Israel kukiuka mara kwa mara sheria za kimataifa na kufanya uhalifu wa kivita huko Ghaza.

Licha ya mashinikizo na maandamano hayo kuathiri maamuzi ya nchi za Ulaya lakini inaonekana kwamba bado kuna ugumu kwa serikali za nchi za Ulaya kuipinga moja kwa moja Israel. Wakati nchi nyingi za Umoja wa Ulaya zimekuwa zikionekana zikikosoa sera za Israel, hasa katika ukiukaji wa haki za binadamu na mashambulizi dhidi ya raia huko Ghaza, kutokana na mashinikizo ya wananchi wa Ulaya, lakini  bado serikali hizo zinaendelea kutoa msaada wa kijeshi kwa Israel. Kwa upande mmoja, nchi za Ulaya zinakosoa jinai za kivita za Israel na zinazungumzia kukata uhusiano; lakini kwa upande mwingine, zinaendelea kuumiminia silaha utawala katili wa Tel Aviv na zinaendeleza uhusiano wa kiuchumi na kibiashara na Israel. Misimamo hiyo na kindumilakuwili imewafanya baadhi ya maafisa wa Ulaya kueleza wasiwasi wao kuhusu mgogoro wa kibinadamu huko Ghaza na kutoa mwito wa kushinikizwa zaidi Israel, lakini kivitendo hawajaonyesha nia kubwa ya kupunguza uungaji mkono wa kijeshi kwa Israel kutokana na maslahi yao ya kiuchumi, na bado zinauhesabu utawala wa Kizayuni kuwa ni mshirika wao muhimu.

Hali hii inaakisi migongano ya kimsingi katika sera za Ulaya kuhusu Israel na Palestina. Inaonekana kwamba maadamu maslahi na mahusiano ya kiuchumi na Israel yanaendelea kupewa kipaumbele, basi hakuna mabadiliko ya kweli yatakayoweza kuonekana katika sera za nchi za Ulaya kuhusu Palestina; suala ambalo linawakasirisha sana walipa kodi wavuja jasho huko Ulaya.

Your Comment

You are replying to: .
captcha