Hamas imeeleza katika taarifa kwamba, kitendo hicho cha kifidhuli kinachochea moja kwa moja hisia za Umma wa Kiislamu na Kiarabu na ni ukiukaji mkubwa wa sheria na desturi za kimataifa, na kwa mara nyingine tena kinadhihirisha mwingiliano kamili na ushiriki wa serikali ya sasa ya Marekani katika jinai za utawala huo ghasibu dhidi ya watu, ardhi na maeneo matakatifu ya Wapalestina.
Hamas imesisitiza kuwa, Ukuta wa Buraq ni sehemu isiyoweza kutenganishwa na Msikiti wa Al-Aqsa, utaendelea kubakia kuwa wa Kiislamu; na njama za utawala wa kizayuni na waungaji mkono wake za kutaka kubadilisha utambulisho wake wa kihistoria na Kiislamu hazitafanikiwa.
Mwishoni mwa taarifa yake hiyo, harakati hiyo ya ukombozi wa Palestina imetahadharisha kuwa, mawe yaliyosafika ya Msikiti wa Al-Aqsa yatazuia majaribio yoyote ya kichokozi ya Wazayuni na kusambaratisha tamaa na njozi za watu wenye misimamo mikali dhidi ya istiqama na Muqawama wa wananchi wa Palestina.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio jana asubuhi aliwasili Palestina inayokaliwa kwa mabavu (Israel) sambamba na kuanza kikao cha dharura cha wakuu wa nchi za Kiislamu kinachofanyika nchini Qatar.
Gazeti la Kizayuni la Ma'ariv limeripoti kuwa Rubio aliwasili Palestina inayokaliwa kwa mabavu Jumapili asubuhi kwa madhumuni ya kukutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa Kizayuni akiwemo waziri mkuu Benjamin Netanyahu, rais Isaac Herzog, na familia za mateka Waisrael.
Kabla ya kuelekea ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu zilizopachikwa jina bandia la Israel, Rubio alidai kuwa serikali ya Marekani haikufurahishwa na shambulio la anga dhidi ya Qatar, lakini pamoja na hayo, shambulio hilo halitaathiri uhusiano wa Marekani na Israel.../
Your Comment