17 Julai 2024 - 12:10
Syed Abdul Malik al-Houthi: Imam Hussein (a.s) alifanya ijtihada za kuuokoa umma wa Kiislamu kutoka katika Udikteta wa Yazid

Kiongozi wa harakati ya Ansarullah ya Yemen amesema: Imam Hussein (a.s) alijitahidi kuuokoa Umma wa Kiislamu kutokana na utawala wa kiimla wa Yazid, jambo ambalo lilikuwa ni hatari kwa dini na kubakia kwake na kuichafua jamii kifisadi.

Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (a.s) - ABNA - "Syed Abdul Malik Badr Al-Din Al-Houthi", Kiongozi wa Ansarullah ya Yemen, alisema katika hotuba yake katika Mnasaba wa A'shura: "Imam Hussein (as) alifanya ijtihada kuuokoa Umma wa Kiislamu kutokana na udikteta wa Yazid, udikteta ambao ulikiwa ni hatari kwa Dini na kubakia kwake na kuitumbukiza jamii kwenye ufisadi.

Kiongozi wa Harakati ya Ansarullah ya Yemen aliongeza kwa kusema: "Suala la Palestina ndilo tatizo na maafa makubwa zaidi duniani, na uga wa makabiliano dhidi ya maadui (wa Umma wa Kiislamu) Israel na Marekani ni uga ambao Umma wote wa (Kiislamu) lazima ushiriki katika hilo."

Akizungumzia ushirikiano wa utawala wa Saudia na maadui wa Umma wa Kiislamu (Israel na Marekani), al-Houthi alisema: "Tunashuhudia hali ya ushirikiano wa wazi kabisa na utumishi kwa maadui (wa Umma wa Kiislamu) kati ya Serikali mbalimbali na Tawala za mamluki, na juu yake ni Qarun wa zama hizi, Utawala wa Saudia.

Kuongezeka kwa uchokozi wa Saudia dhidi ya watu wetu kulikofanyika baada ya Marekani kuamuru Utawala huo mamluki kuitumikia Israel.

Kuhusiana na hilo aliongeza kwa kusema: "Ninaishauri Saudi Arabia isikilize maonyo na nara za taifa letu na kuacha njia yake potovu (na ya kimakosa) ambayo inaifanya ipendelea na kuelemea kwa Marekani na Israel dhidi ya Mwenyezi Mungu, Uislamu, Dini na Hekima; kwa sababu Mwenyezi Mungu atamdhalilisha na kumdunisha mtawala (twaghuti) jeuri wa zama hizi, yaani Marekani, kupitia mikononi mwa taifa letu.

Al-Houthi alisema: "Mwenyezi Mungu atazitokomeza dhulma za washirika wa Marekani na kuharibu uwezo wao kwa kupitia mikono ya watumishi wake watiifu, ushindi katika hilo ni wa Taifa la Palestina na Taifa letu.

Aliongeza: "Moja ya matokeo ya operesheni zetu, ambayo ni ya kushangaza na isiyo ya kawaida kwa maadui, ilikuwa ni kutimuliwa kwa manuari kubwa ya kubeba ndege za kivita ya Marekani iitwayo (Eisenhower) kutoka Bahari ya Shamu (Red Sea).

Al-Houthi pia alisisitiza: "Tunalihakikishia Taifa la Palestina ya kwamba hatutaacha juhudi zozote katika kuwahami na kuwaunga mkono".