19 Julai 2024 - 19:25
Sisitizo la viongozi wakuu wa Iran na Saudia la kuimarisha uhusiano baina ya nchi zao

Mohammed bin Salman, mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia na Massoud Pezeshkian, rais mteule wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, wamezungumza kwa simu na kutilia mkazo umuhimu wa kuendeleza ushirikiano kati ya Tehran na Riyadh.

Katika mazungumzo hayo Bin Salman amempongeza Masoud Pezeshkian kwa kuchaguliwa kuwa rais wa 9 wa Jamhuri ya Kiislamu kuchukua nafasi ya marhum shahid Rais Ebrahim Raisi na kumuombea dua ya ufanisi na mafanikio katika kazi zake. Mrithi huyo wa kiti cha ufalme za Saudia amesema kuwa Riyadh inataka kuimarisha uhusiano na ushirikiano wake na Tehran kwa manufaa ya nchi na mataifa haya mawili na dunia nzima kiujumla. Kwa upande wake, Masoud Pezeshkian amemshukuru mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia kwa dua zake nzuri na kutilia mkazo wajibu wa kuimarishwa zaidi na zaidi uhusiano baina ya nchi hizi mbili kubwa za Kiislamu. Uhusiano baina ya Iran na Saudia umeimarika katika katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni na hususan wakati wa serikali ya 13 ya Jamhuri ya Kiislamu iliyoongozwa na Rais Ebrahim Raisi na waziri wake wa mambo ya nje, Hossein Amir-Abdollahian waliokufa shahidi katika ajali ya helikopta iliyotokea nchini Iran mwezi Mei mwaka huu. Mara kwa mara viongozi wakuu wa nchi hizi mbili wamekuwa wakitoa matamshi ya kutilia mkazo wajibu wa kulindwa hali iliyopo na kuimarishwa zaidi na zaidi uhusiano wa pande mbili kwa manufaa ya eneo hili na dunia nzima kiujumla hasa Ulimwengu wa Kiislamu.

Hata katika kampeni za uchaguzi, rais mteule wa Iran, Masoud Pezeshkian alikuwa anatilia mkazo wajibu wa kuimarishwa uhusiano wa Tehran na nchi jirani na kuendelezwa siasa za serikali ya 13 ya shahid Ebrahim Raisi. Hii ni kwa sababu uhusiano mzuri baina ya nchi za eneo hili ni kwa manufaa ya mataifa yote na ni kwa madhara ya maadui hasa utawala wa Kizayuni na madola ya kibeberu. Mfano wa wazi ni yale yaliyotokea baada ya kufikiwa makubaliano ya kurejesha uhusiano baina ya Iran na Saudi Arabia yaliyosimamishwa na China na ambayo yalifikiwa kwa juhudi kubwa za marhum sahid Amir-Abdullahian, waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Iran. Baada ya makubaliano hayo, nchi za Kiarabu zilizokuwa zimesimamisha uhusiano wao na Tehran kwa kuifuata Saudi Arabia, nazo zimetangaza kurejesha uhusiano wao na Jamhuri ya Kiislamu jambo ambalo ni mafanikio makubwa kwa ajili ya ustawi wa kisiasa na kiuchumi wa eneo hili zima. 

Iran na Saudia ni nchi mbili kubwa za Kiislamu zenye utajiri wa mafuta. Kuwepo ushirikiano baina yao katika nyuga zote, ni kwa manufaa ya Ulimwengu wa Kiislamu na ni kwa madhara ya madola yote yasiyowatakia kheri Waislamu duniani. Ni kwa sababu hiyo ndio maana kadiri uhusiano wa Iran na nchi za Kiarabu unavyoimarika, ndivyo nyoyo za Waislamu na wapenda haki duniani zinavyozidi kufurahi na kufarijika.
Suala jingine muhimu ni kwamba, dunia nzima inaelewa kuwa, kadhia ya ukombozi wa Palestina ni suala la kimsingi katika siasa za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kiasi kwamba, wagombea wote wa uchaguzi wa 14 wa hivi karibuni nchini Iran, walikuwa na kauli moja kuhusu ukombozi wa taifa linalodhulumiwa la Palesitna. Katika upande wa pili, kuanzia tarehe 7 Oktoba, 2023 hadi hivi sasa, utawala wa Kizayuni unafanya mauaji ya kutisha dhidi ya wananchi wasio na ulinzi wa Palesitna hasa wa Ukanda wa Ghaza. Ukatili huo wa Israel ulianza kipindi ambacho Saudia ilikuwa kwenye mchakato wa kutangaza uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni, lakini baada ya Oktoba 7, 2023, mchakato huo umesambaratika kabisa na Saudi Arabia imekuwa ikisema mara kwa mara kwamba Israel lazima ikomeshe jinai zake huko Ghaza. Bila ya shaka yoyote jambo hilo linawafurahisha Waislamu na wapenda haki duniani na linakwenda kwenye njia ile ile ya ukombozi wa Palestina ambao ni msingi mkuu wa siasa za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Hayo yote ni katika matunda ya kuweko uhusiano mzuri baina ya Iran na nchi za Kiarabu ikiwemo Saudia. Kiujumla ni kwamba, siasa kuu za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kuishi kwa usalama na nchi nyingine hasa nchi jirani kwani inaamini kuwa ni katika mazingira ya utulivu na usalama tu ndipo yanapoweza kupatikana maendeleo na ustawi kwa mataifa ya dunia na ndio maana muda wote huo haipotezi fursa yoyote ya kuwa na uhusiano mzuri na nchi nyingine hasa za eneo hili na nchi za Kiislamu.

342/