Shirika la habari la Palestina (SAMA) limeripoti kuwa, Wapalestina 85 wameuawa shahidi na wengine 250 kujeruhiwa katika mashambulizi mtawalia ya utawala wa Israel katika mji wa Khan Yunis kusini mwa Ukanda wa Gaza.
Duru za habari za Palestina pia zimeashiria kuendelea mashambulizi ya jeshi la utawala wa Kizayuni katika maeneo ya katikati mwa mji wa Khan Yunis na kueleza kuwa, kitongoji cha al Qarara huko kaskazini mwa mji wa Khan Yunis pia kimeshambuliwa na jeshi la Israel. Jeshi la Israel pia limelishambulia gari lililokuwa limewapakia wakimbizi wa Kipalestina katika eneo la Bani Suhaila katika mji wa Khan Yunis.
Ndege za kivita za Israel pia zimeyashambulia maeneo ya Sheikh Nassir, al Balad, al Mutahan, Absan al Kabirah katika mji wa Khan Yunis.
Utawala wa Kizayuni wa Israel umewaua takriban Wapalestina 39,006 wa Gaza, wengi wao wakiwa wanawake, watoto na vijana. Wapalestina wengine 89,818 wamejeruhiwa.
342/