Benjamin Netanyahu, siku ya Jumatano alihutubia Kongresi ya Marekani. Katika hotuba yake ya kujitoa kimasomaso, ya kujaribu kuelekeza kidole cha tuhuma kwa wengine na ya kuzibabaisha fikra za umma ulimwenguni kuhusiana na jinai za kinyama zinazoendelea kufanywa na utawala wa Kizayuni huko Ghaza, Netanyahu alisema: "maadui zetu ni maadui zenu na ushindi wetu ni ushindi wa Marekani".
Netanyahu, ambaye katika hotuba yake hiyo alijikita zaidi kuishambulia Iran kwa maneno alidai kuwa Iran ndiyo muungaji mkono mkuu wa makundi (ya Muqawama) yanayoipinga Israel katika eneo, hivyo inapasa kukabiliana nayo.
Waziri mkuu huyo wa utawala haramu wa Israel, ambaye hivi sasa anaandamwa na mashinikizo ya nchi mbalimbali, jumuiya za kimataifa na mashirika ya kutetea haki za binadamu kwa kuhusika na uhalifu wa kivita huko Ghaza, alidai kuwa Iran inafadhili kifedha maandamano yanayofanyika Marekani dhidi ya Israel.Katika sehemu nyingine ya hotuba yake iliyokuwa ikishangiliwa mara kwa mara na wajumbe wa Kongresi ya Marekani, Netanyahu alizungumzia tena njozi ya alinacha unayoota utawala wa Kizayuni kuhusu Baitul Muqaddas na akasema: "Jerusalem (Baitul Muqaddas) ni mji mkuu wa milele wa Israel na hautagawanywa kamwe".
Netanyahu alitoa matamshi na madai yake hayo, wakati maandamano makubwa yalikuwa yakifanyika karibu na jengo la Kongresi na maeneo mengine ya Washington kupinga na kulaani jinai za utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Ghaza.
Hotuba ya Netanyahu katika Bunge la Marekani ilisusiwa na wabunge kadhaa wa nchi hiyo. Nancy Pelosi, spika wa zamani wa Baraza la Wawakilishi la Marekani amesema kuhusiana na hilo kwamba, hotuba ya Netanyahu ni hotuba mbaya zaidi kuwahi kutolewa na kiongozi wa kigeni mbele ya Kongresiya nchi hiyo. Katika mjibizo wake kwa hotuba ya Netanyahu katika Kongresi ya Marekani, Riyadh Mansour, mwakilishi wa Palestina katika Umoja wa Mataifa amesema, hotuba hiyo imejaa uongo na kauli za kujionyesha na kujifanya mdhulumiwa. Osama Hamdan, afisa mwandamizi wa harakati ya Hamas yeye amesema, hotuba ya Netanyahu imejaa uwongo kuhusu urejeshaji wa mateka na uhalalishaji wa jinai za kinyama zinazofanywa na utawala huo. Harakati yenyewe ya Hamas imetangaza katika taarifa yake kwamba, Washington imetilia mkazo na kuthibitisha kuwa ni mshirika katika vita na jinai dhidi ya wakazi wa Ghaza kwa kuendelea kutoa uungaji mkono wa kijeshi na kisiasa kwa utawala wa Kizayuni na kumpatia fursa Netanyahu ya kuhutubia.Pamoja na yote hayo inapasa tuseme kuwa, hotuba aliyotoa Netanyahu siku ya Jumatano katika Bunge la Marekani imeonyesha kwamba Washington, ambayo ni mshirika wa kistratejia wa Israel, inaendelea kutoa uungaji mkono mkubwa wa kijeshi na kisiasa kwa Tel Aviv; na licha ya kutangazwa na Umoja wa Mataifa kwamba Israel inafanya mauaji ya kimbari huko Ghaza ingali inakanusha ukweli huo. Hatua ya Washington ya kuiunga mkono Tel Aviv bila kuhoji chochote ni tafsiri ya wazi kabisa ya kuupa kibali na ridhaa kamili utawala wa Kizayuni ya kuendeleza jinai zake, hususan mauaji ya kimbari dhidi ya watu wa Ghaza na kutumia silaha ya kuwadhikisha na kuwaweka na njaa Wapalestina hao madhulumu.
Hayo yanafanyika wakati nchi nyingi na mashirika ya kutetea haki za binadamu kama vile Amnesty International zinataka Marekani ikomeshe kuipatia silaha Israel inazotumia kuulia Wapalestina. Lakini pamoja na yote hayo, tajiriba ya karibu miezi 10 ya Muqawama wa wananchi wa Palestina imeonyesha kuwa uungaji mkono wa kijeshi na kisiasa wa Marekani na washirika wake wa Ulaya kwa utawala wa Kizayuni haujabadilisha hali ya vita vya Ghaza, na makundi ya Muqawama yameweza kusimama imara dhidi ya uchokozi na mashambulizi ya kinyama ya utawala wa Kizayuni kwa nguvu na uwezo kamili, kiasi kwamba viongozi wa kijeshi wa utawala wa Kizayuni na waungaji mkono wao pia wamekiri kuwa wameshindwa na wamegonga mwamba katika vita hivyo haribifu na vilivyowasababishia gharama kubwa.../
342/