22 Februari 2025 - 19:36
Kilele cha utayarifu wa Jeshi la Iran kwa ajili ya kukabiliana na tishio la adui

Pembezoni mwa hatua ya mwisho ya mazoezi ya kijeshi yaliyopewa jina la Mtume Mtukufu wa 19 (SAW) ya Vikosi vya Jeshi la Nchi Kavu vya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC), Meja Jenerali Mohammad Bagheri, Mkuu wa Majeshi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, vikosi vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu viko katika kilele cha utayarifu.

Amesema: "Likitokea kosa lolote la adui, amani ya utawala ghasibu na wale wote wanaouzatiti kwa silaha na kushiriki katika operesheni zake, itakuwa hatarini."

Katika miezi ya hivi karibuni, adui Mzayuni amekuwa akitoa madai mara kadhaa kuhusu kudhoofisha nguvu za kijeshi za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Adui huyo pia amedai kuwa amejiandaa kushambulia vituo vya nyuklia vya Iran.

Serikali mpya ya Marekani pia imezungumzia suala hilo na kudai kuwa utawala wa Kizayuni wa Israel uko tayari kuishambulia Iran. Vyombo vya habari pia vimejikita katika propaganda hizo za adui na kutoa madai na vitisho hivyo.

Lakini swali ni kwamba, nini hakika na ukweli wa madai haya?

Ukweli ni kwamba madai ya kudhoofika nguvu ya kijeshi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran yanatolewa katika muktadha wa vita vya kisaikolojia dhidi ya Iran. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iko tayari kutekeleza Operesheni Ahadi ya Kweli 3, lakini hadi sasa imejizuia kufanya hivyo ili kuzuia kuenea vita katika eneo la Magharibi mwa Asia na kwa shabaha ya kurejesha amani na usalama katika eneo hilo.

Ukweli mwingine ni kwamba, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina nguvu kubwa za kijeshi na imepata uwezo wa kujitegemea katika uga wa ulinzi.

Wakati utawala wa Kizayuni ulipoonyesha uwezo wake kamili wa kijeshi katika vita vya miezi 15 dhidi ya Gaza na Lebanon, Jamhuri ya Kiislamu ilikhitari kwamba itadhihirisha uwezo wake wa kijeshi katika vita vikubwa pekee. Kwa hivyo, madai ya kudhoofika nguvu za jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni ya uongo, na hata mashirika ya ujasusi ya Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel yanajua vyema uwezo wa kijeshi wa Iran.

Ukweli mwingine ni kwamba, kinyume na propaganda zilizoenezwa za adui Mzayuni kuhusu uharibifu wa nguvu za ulinzi wa anga za Iran, uharibifu huo haukuwa mkubwa kama inavyodaiwa. Si hayo tu, bali hata wakosoaji wa baraza la mawaziri la Benjamin Netanyahu na vyombo vya habari vya Kizayuni vimekuwa vikitangaza mara kwa mara kwamba utawala huo umeshindwa kutoa pigo kubwa kwa Iran na umefeli mbele ya Jamhuri ya Kiislamu.

Akizungumzia suala hilo, Meja Jenerali Bagheri, Mkuu wa Majeshi ya Jeshi la Iran amesema kwamba ulinzi wa anga wa Jamhuri ya Kiislamu uko katika hali ya juu ya utayarifu na kwamba uharibifu mdogo lililoupata umerekebishwa kikamilifu.

La muhimu ni kwamba leo hii, kinyume na propaganda zinazoenezwa na maadui, vikosi vya jeshi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran viko kwenye kilele cha utayarifu. Mazoezi ambayo yamekuwa yakifanyika katika miezi ya hivi karibuni hapa nchini pia yanalenga kuongeza utayarifu wa vikosi vya jeshi.

Wakati huo huo, kuboresha silaha na kutengeneza silaha mpya na za kisasa pia ni ajenda inayoendelea kufanyiwa kazi kwa sasa. Mkuu wa Majeshi ya Iran pia amesema kuhusiana na suala hilo kwamba: "Ulinzi wa anga wa majeshi ya Jamhuri ya Kiislamu uko kwenye kilele cha utayarifu wa mashambulizi, na utengenezaji wa makombora pia unafanywa kwa wingi na kwa ubora wa juu zaidi bila ya kusita."

Akizungumzia mipango kabambe ya utumiaji wa ndege ndogo zisizo na rubani katika vitengo mbalimbali vya vikosi vya jeshi, Meja Jenerali Mohammad Bagheri amesema: "Katika hatua ya kwanza, vikosi vya Jeshi la Nchi Kavu vya IRGC na Jeshi la Taifa vitawezeshwa kwa ndege hizo ndogo zisizo na rubani na vitengo vingine vitapewa uwezo huo kulingana na mahitaji na udharura wa kikazi."

342/