18 Machi 2025 - 23:30
Tusiwe wavivu ndani ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhan, na tusichoke kuomba Maghfira na Msamaha

Kila kizuri unachokifanya ndani ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhan, ni thawabu.Hata pumzi zetu tunapopumua ndani ya Mwezi huu, hilo linahesabiwa kuwa ni ibada, na hata kulala kwetu na usingizi wetu ndani yake pia ni ibada. Sisi ni wageni wa Mwenyezi Mungu ndani yake.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Ahlul-Bayt (a.s) -ABNA-, Samahat Sheikh Mohammad Abdu, Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini wa Jumuiya ya Shia Ithna Ashari Tanzania (T.I.C), amewakumbusha Waumini wa Kiislamu juu ya Fadhila za Mwezi huu Mtukufu wa Ramadhan, na kuwahimiza wasiochoke wala kuwa na uvivu wa aina yoyote ndani yake katika kufanya ibada mbalimbali, na kuomba maghfira na msamaha kwa Mwenyezi Mungu (s.w.t).

Amefafanua zaidi katika darsa lake akisema: Kila kizuri unachokifanya ndani ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhan, ni thawabu. Hata pumzi zetu tunapopumua ndani ya Mwezi huu, hilo linahesabiwa kuwa ni ibada, na hata kulala kwetu na usingizi wetu ndani yake pia ni ibada. Na dua zetu ni zenye kujibiwa ndani yake, kwa sababu sisi ni wageni wa Mwenyezi Mungu ndani yake, na Mwenyezi Mungu ndiye Mwenyeji wetu ndani yake, na Mwenye kutukirimu na kujibu kila aina ya maombi yetu na shida zetu zote.

Mtume wetu Muhammad (s.a.w.w) anatwambia:

Tusiwe wavivu ndani ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhan, na tusichoke kuomba Maghfira na Msamaha

"فَاسْأَلُوا اللَّهَ رَبَّکُمْ بِنِیَّاتٍ صَادِقَةٍ وَ قُلُوبٍ طَاهِرَةٍ أَنْ یُوَفِّقَکُمْ لِصِیَامِهِ وَ تِلَاوَةِ کِتَابِهِ"

"Basi muombeni Mwenyezi Mungu, Mola wenu Mlezi, kwa nia ya kweli na nyoyo safi (zilizotakasika, pasina kuwa na shaka yoyote, na zinazotambua kuwa anayeombwa ni Mwenyezi Mungu na maombi haya yanakwenda Kwake moja kwa moja), akupeni taufiki (akuwezesheni) katika kuufunga - Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan - na kukisoma Kitabu Chake".

Vile vile Mtume (s.a.w.w) anasema katika Hotuba yake:

Tusiwe wavivu ndani ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhan, na tusichoke kuomba Maghfira na Msamaha

"أَیُّهَا النَّاسُ مَنْ فَطَّرَ مِنْکُمْ صَائِماً مُؤْمِناً فِى هَذَا الشَّهْرِ کَانَ لَهُ بِذَلِكً عِنْدَ اللَّهِ عِتْقُ نَسَمَةٍ وَمَغْفِرَةٌ لِمَا مَضَى مِنْ ذُنُوبِهِ، قِیلَ یَا رَسُولَ اللَّهِ فَلَیْسَ کُلُّنَا یَقْدِرُ عَلَى ذَلِكَ، فَقَالَ (صلى الله عليه وآله وسلم) اتَّقُوا النَّارَ وَلَوْ بِشِقِّ تَمْرَةٍ اتَّقُوا النَّارَ وَلَوْ بِشَرْبَةٍ مِنْ مَاء"

"Enyi watu! Yeyote miongoni mwenu atakayemfturisha Muumini (mmoja tu) aliyefunga Swaumu katika Mwezi huu, atalipwa na Mwenyezi Mungu (malipo kama yale ambayo mtu atalipwa kwa) kumuacha huru mja Wake, na atamsamehe dhambi zake zilizopita.

Baadhi ya Maswahaba wakasema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Sio sote hatuna uwezo wa kuifanya hivyo. Mtume (s.a.w.w) akasema: Uogopeni (uepukeni) moto wa Jahannam walau kwa kumfuturisha mtu (aliyefunga) hata kwa nusu (punje) ya tende,  uogopeni (uepukeni) moto wa Jahannam walau kwa kumfuturisha (aliyefunga) hata kwa funda la maji".

Pia Mtume wetu Muhammad (s.a.w.w) anaendelea kutufundisha na kutuusia akisema:

Tusiwe wavivu ndani ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhan, na tusichoke kuomba Maghfira na Msamaha

"مَن حَسَّنَ مِنکُم في هذَا الشَّهرِ خُلُقَهُ کانَ لَهُ جَوازاً عَلَى الصِّراطِ یَومَ تَزِلُّ فیهِ الأَقدامُ"

"Yeyote miongoni mwenu atakayeboresha (na kuifanya iwe nzuri) tabia yake katika Mwezi huu, huyo atakuwa na njia ya kupta na (kuvuka na) katika Daraja la Sirat, siku ambayo miguu (ya watu itakuwa) ikiteleza".

Tags

Your Comment

You are replying to: .
captcha