24 Machi 2025 - 18:18
Source: Parstoday
Diplomasia hai ya Iran katika kukabiliana na migogoro inayoibuliwa na utawala wa Kizayuni katika eneo

Seyyed Abbas Araghchi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amezungumzia matukio ya eneo, yakiwemo ya Palestina na Yemen katika mazungumzo yake ya simu na Mawaziri wenzake wa Mashauri ya Kigeni wa Saudi Arabia na Misri na kubadilishana nao mawazo jinsi ya kukabiliana na migogoro inayoibuliwa mara kwa mara na utawala wa Kizayuni katika eneo.

Katika mazungumzo yake na Faisal bin Farhan, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Saudi Arabia, pande mbili  zimesisitiza ulazima wa kuwepo uratibu na maingiliano ya karibu kati ya nchi za eneo ili kuzuia kushadidi migogoro katika eneo hili la kistratijia.

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amelaani vikali jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya wananchi wasio na ulinzi wa Palestina huko Gaza na kusisitiza udharura wa kuchukuliwa hatua za pamoja na nchi za Kiislamu ili kukomesha jinai hizo. Araghchi pia amelaani vikali hujuma za kijeshi za Marekani na Uingereza dhidi ya Yemen na mauaji ya wanawake na watoto wasio na hatia na uharibifu wa miundombinu ya nchi hiyo, na kuukumbusha ulimwengu wa Kiislamu wajibu wake wa pamoja wa kuwaunga mkono Waislamu wa Yemen.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia naye katika mazungumzo hayo ya simu ameelezea msimamo wa nchi yake wa kulaani vikali hujuma ya Israel na kusisitiza ulazima wa kuwepo uratibu na maingiliano ya karibu kati ya nchi za eneo ili kuzuia kushadidi mgogoro huo.

Araghchi katika mazungumzo yake na Badr Abd al-Ati, Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri, amelaani kuanzishwa tena mashambulizi ya Israel dhidi ya Gaza, mauaji ya raia na kuzuiwa misaada ya kimataifa ya kibinadamu kuingia Gaza kinyume na makubaliano ya usitishaji vita, na kutoa wito wa kuchukuliwa hatua za haraka na jamii ya kimataifa ili kukomesha uchochezi wa vita wa utawala wa Kizayuni katika eneo.

Katika mazungumzo hayo ya simu, Badr Abdul Ati amesema kushadidi vita huko Gaza, Yemen na Lebanon ni jambo linalotia wasiwasi mkubwa na kusisitiza umuhimu wa kufanyika mashauriano na juhudi za kidiplomasia ili kuzuia kuharibika zaidi mambo katika eneo zima. Pande hizo pia zimesisitiza juu ya kuendelea mawasiliano na mashauriano kuhusu matukio ya eneo.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inafuatilia malengo kadhaa katika mashauriano yake ya kikanda na kidiplomasia na nchi za ulimwengu wa Kiislamu dhidi ya utawala wa Kizayuni na mshirika wake mkuu Marekani.

Diplomasia hai ya Iran katika kukabiliana na migogoro inayoibuliwa na utawala wa Kizayuni katika eneo

Kuwaunga mkono wananchi wa Palestina na kujaribu kukomboa ardhi zinazokaliwa kwa mabavu ni moja ya malengo muhimu ya kidiplomasia ya Iran katika kukabiliana na utawala ghasibu wa Israel. Kupitia ushirikiano wa kieneo, Iran inataka kutimiza lengo hilo na inajaribu kuimarisha harakati za muqawama wa Palestina na kupambana na vitendo vya unyakuzi wa ardhi na uvamizi wa Wazayuni.  Iran daima imekuwa ikisisitiza juu ya kuimarishwa muqawama dhidi ya utawala wa Kizayuni.

Katika hali ya sasa ya eneo, na kwa kuzingatia siasa za Wazayuni za kuibua ghasia na vita katika eneo, jambo ambalo linaweza kuwa na nafasi muhimu katika kuimarisha safu ya muqawama na kuunga mkono wananchi wa Palestina na Lebanon ni umoja na mshikamano wa ulimwengu wa Kiislamu. Bila shaka, la muhimu zaidi, ni kwamba nchi za Kiislamu za eneo, ambazo raia wao wengi wanaunga mkono watu wa Palestina na Lebanon, zinaweza kuwa na nafasi muhimu katika kuutenga utawala wa Kizayuni.

Iran, ikiwa mhusika mkuu katika matukio ya kieneo, daima imekuwa na nafasi muhimu katika kuifahamisha jamii ya kimataifa jinai zinazofanywa na utawala wa Kizayuni, na bila shaka suala hilo sasa linazingatiwa zaidi ulimwenguni kufuatia operesheni ya "Kimbunga cha al-Aqsa." Kutokana na juhudi za kidiplomasia za Iran, jamii ya kimataifa hii leo haiwezi tena kupuuza hali ya Palestina, Lebanon na Yemen, jambo ambalo bila shaka ni matokeo ya kutekelezwa kivitendo misingi ya kibinadamu na kimaadili ya siasa za kigeni za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Kupitia ushirikiano na mshikamano, nchi za eneo hili bila shaka zina uwezo mkubwa wa kukabiliana na siasa pamoja na hatua za Marekani na utawala wa Kizayuni za kuibua mivutano ya kikanda, na hilo litathibiti tu kwa kuimarishwa umoja na kuepuka kuwategemea wageni katika kila jambo, na hasa katika kudhamini usalama.

Diplomasia hai ya Iran katika kukabiliana na migogoro inayoibuliwa na utawala wa Kizayuni katika eneo

Kwa kutilia maanani duru mpya ya juhudi za pamoja za kuibua migogoro zinazofanywa na Wamagharibi na Wazayuni, kuna ulazima wa nchi za eneo kushirikiana katika kukabiliana na uingiliaji wa kigeni na kufikia amani ya kudumu.

Matukio ya Lebanon, Syria, Palestina na Yemen yanathibitisha ukweli kwamba njia muhimu zaidi ya kukomesha uingiliaji wa kigeni ni kuendelezwa mashauriano ya kidiplomasia kikanda. Mashauriano haya, ambayo yanafanyika kupitia mhimili wa Iran, yamekuwa na matokeo chanya katika fikra za waliowengi katika ulimwengu wa Kiislamu, na bila shaka yanaweza kuwa na nafsi muhimu katika kurejesha uthabiti na kupunguza mivutano katika eneo.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inazingatia pakubwa masuala ya kibinadamu na kimaadili kama msingi muhimu wa siasa zake za kigeni. Kuzingatia haki halali za wananchi wa Palestina na kukabiliana na siasa za kujipanua utawala ghasibu wa Wazayuni na waungaji mkono wao wa Marekani na Magharibi ni miongoni mwa vigezo vikuu vya diplomasia ya kieneo ya Iran ambavyo vimekuwa vikifuatiliwa kwa karibu na serikali ya Tehran katika miaka ya hivi karibuni.

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha