26 Machi 2025 - 15:22
Source: Parstoday
Iran yazionya nchi jirani: Jihadharini na ufitinishaji na ufarakanishaji wa Marekani

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amezungumzia tuhuma zilizotolewa na viongozi wa Marekani kuhusiana na kuiwekea mashinikizo Iran na akasema: "inavyotarajiwa, nchi jirani na marafiki zitajihadhari na ufitinishaji na ufarakanishaji unaofanywa na Marekani".

Sayyid Abbas Araqchi, ametoa indhari hiyo katika mazungumzo aliyofanya kwa njia ya simu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq Fuad Hussein ambapo wawili hao wamejadili matukio yanayojiri hivi sasa katika eneo.

Katika mazungumzo hayo, mawaziri wa mambo ya nje wa Iran na Iraq wamejadili na kubadilishana mawazo kuhusu matukio yanayojiri hivi sasa katika eneo kufuatia kuanza tena mashambulizi ya kinyama ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Ghaza na Lebanon kwa upande mmoja na hujuma za kijeshi za Marekani dhidi ya Yemen kwa upande mwingine.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amelaani vikali mwendelezo wa mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala wa Kizayuni huko Ghaza na uchokozi wake wa mara kwa mara dhidi ya Lebanon - ambao unafanyika kwa kukiuka waziwazi makubaliano ya kusitisha vita na kwa baraka kamili za Marekani - pamoja na mauaji ya wanawake na watoto wasio na hatia, na akatoa wito wa kuchukuliwa hatua za haraka na jamii ya kimataifa, hususan nchi za eneo na za Kiislamu, ili kukomesha jinai na uchokozi huo na kuzuia kuvurugika zaidi amani katika eneo zima.

Akiashiria hatari kubwa inayoweza kusababishwa na Marekani kwa kuvitumia vibaya vituo vyake vya kijeshi vilivyoko katika nchi za eneo na anga za nchi hizo ili kuanzisha uchokozi na uvamizi dhidi ya mataifa ya eneo hili, Araghchi amesisitizia udharura wa nchi zote za eneo kuchukua hatua zinazohitajika ili kulinda mamlaka ya kujitawala ya kitaifa na kuzuia ardhi na suhula zao kutumiwa na vikosi vya majeshi ya kigeni kwa ajili ya kuvuruga usalama wa nchi zingine.

Katika mazungumzo hayo na mwenzake wa Iraq, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameashiria pia vikwazo haramu vya Marekani dhidi ya sekta ya mafuta ya Iran na akabainisha kwamba, madai na tuhuma zinazotolewa na viongozi wa Marekani kwa ajili ya kuiwekea mashinikizo Iran hazina msingi wala itibari yoyote, na matarajio ni kwamba nchi jirani na marafiki zitajihadhari na ufitinishaji na ufarakanishaji unaofanywa na Marekani ambao hauna nia nyingine isipokuwa kuharibu uhusiano wa kirafiki baina ya nchi za eneo hili sambamba na kufanikisha malengo ya utawala ghasibu wa Kizayuni.

Kwa upande wake, Fuad Hussein ameeleza wasiwasi mkubwa alionao kutokana na matukio yanayojiri katika eneo na hatari kubwa zinazoweza kusababishwa na kuendelea uchokozi wa kijeshi dhidi ya Ghaza, Lebanon na Syria, na akasisitizia haja ya kuwepo ushirikiano na mtazamo wa pamoja kati ya nchi za eneo ili kusaidia kupunguza mateso ya wananchi wanaodhulumiwa wa Palestina na kuzuia kuhatarishwa amani na utulivu wa eneo zima.../

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha