Hamas imesema hayo kwa mnasaba wa maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Palestina na kusisitiza kuwa: Takriban watoto 19,000 wameuawa shahidi katika Ukanda wa Ghaza, zaidi ya watoto 1,100 wametekkwa nyara na Wazayuni na takriban watoto 39,000 wamepoteza mzazi mmoja au wote wawili.
Imesema: "Utawala wa Kizayuni unaokalia kwa mabavu unalenga watoto katika mashambulizi ya kijinai na uhalifu wa kimfumo, ikiwa ni pamoja na kuwatumia kama ngao za binadamu, kuwanyima elimu na kufanya njama za kuwavua utambulisho wao wa kitaifa katika maeneo ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu na Wazayuni."
Hamas imeongeza kuwa: Jinai za utawala huo ghasibu dhidi ya watoto wa Palestina yakiwemo mauaji ya kukusudia, kuwateka nyara watu, kuwatesa na kuwanyima haki za kimsingi kabisa za kibinadamu. Yote hayo yanahesabiwa ni ukiukwaji mkubwa wa sheria za kimataifa za kibinadamu na ni jinai ambazo hazitafutika ndani ya historia.
Vilevile harakati ya Hamas imetoa mwito wa kuburuzwa mahakama viongozi watenda jinai wa Israel na kufanyike juhudi kubwa za kuwalinda watoto wa Palestina mbele ya jinai za utawala huo ghasibu.
Kwa upande wake, msemaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Palestina UNRWA amesema kuwa, asilimia 51 ya wakaazi wa Ukanda wa Ghaza ni watoto ambao ndio asilimia kubwa zaidi ya wahanga wa hujuma na mashambulizi ya Israel.
342/
Your Comment