5 Aprili 2025 - 23:35
Source: Parstoday
UN: Israel imegeuza theluthi mbili za ardhi ya Ghaza kuwa eneo lisiloruhusiwa kufika

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) imetangaza kuwa, hivi sasa utawala wa Kizayuni wa Israel umewawekea vizuizi Wapalestina vya kutoruhusiwa kufika kwenye takriban theluthi mbili ya eneo la Ukanda wa Ghaza, ama kwa kuyatangaza maeneo makubwa kadhaa ya ukanda huo kuwa ni marufuku kufika au kutoa amri ya kuwalazimisha wananchi hao kuyahama makazi yao.

Miongoni mwa maeneo yaliyowekewa vizuizi hivyo ni eneo kubwa la kusini mwa Rafah, ambapo jeshi la utwala ghasibu wa Israel lilitoa amri mpya kwa Wapalestina ya kuhama makazi yao Machi 31, na kutangaza kuwa linajipanga kurudi ili "kupigana kwa nguvu kubwa".

Vizuizi hivyo vimejumuisha pia sehemu kadhaa za Mji wa Ghaza, ambako wanajeshi wa Kizayuni walianzisha mashambulizi mapya ya ardhini Ijumaa asubuhi ili kupanua kile walichodai kuwa ni "eneo lao la usalama".

Ongezeko hilo la uwekaji vizuizi limeibua moja ya mawimbi makubwa zaidi ya Wapalestina wanaolazimika kuyahama makazi yao kwa sababu ya vita, kwa kuhamisha mamia ya maelfu, huku wengi wao wakiwa tayari wameshalazimika mara kadhaa kuhama sehemu moja na kuhamia sehemu nyengine.

Mnamo Machi 18, utawala wa Kizayuni wa Israel ulianzisha tena vita vya kinyama na mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Ghaza na kuvunja kikamilifu usitishaji mapigano uliodumu kwa miezi miwili kufuatia makubaliano uliyofikia na harakati ya Hamas kwa upatanishi wa serikali iliyopita ya Marekani, Qatar na Misri. 

Waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni Benjamin Netanyahu ametangaza kuwa lengo la kuanzisha tena vita dhidi ya Ghaza ni kuilazimisha Hamas iwaachilie mateka 59 wa Kizayuni waliosalia mkabala wa kuachiwa huru Wapalestina wanaoshikiliwa kwenye jela za Israel na kuruhusu tena misaada kuingizwa huko Ghaza.

Hata hivyo amepinga kikamilifu utawala huo ghasibu kuhitimisha vita na kuondoa majeshi yake yote katika Ukanda wa Ghaza kama ilivyoafikiwa katika mpango wa mapatano uliopendekezwa na Marekani. 

Netanyahu anasisitiza pia kuwa Hamas lazima ipokonywe silaha, takwa ambalo harakati hiyo ya ukombozi wa Palestina imelitaja kuwa ni mstari mwekundu kwake, na vilevile anataka utawala wa Kizayuni uwe na mamlaka ya kudhibiti usalama wa Ghaza, mbali na kuunga mkono takwa la rais wa Marekani Donald Trump la kuwahamisha kwa nguvu Wapalestina wote wa eneo hilo.../

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha