7 Mei 2025 - 21:41
Source: Parstoday
Ansarullah: Mapatano na Marekani hayatazuia mashambulizi ya Yemen dhidi ya Israel

Harakati ya Muqawama ya Ansarullah ya Yemen imesema kuwa kusitishwa kwa mashambulizi ya anga ya Marekani dhidi ya Yemen mkabala wa kusitisha mashambulizi dhidi ya meli za kivita za Marekani katika Bahari ya Shamu hakutabadilisha msimamo wa Yemen kuhusu kushambulia Israel.

Msemaji wa Ansarullah, Mohammed Abdul-Salam, amesisitiza kuwa Vikosi vya Jeshi la Yemen vitaendelea kushambulia ngome za utawala haramu wa Israel kuonyesha mshikamano na Wapalestina katika Ukanda wa Gaza ulioathiriwa na vita.

Abdul-Salam amesema kuwa mkataba na Marekani "hauhusiani na msimamo wetu wa kuwaunga mkono watu wa Gaza," akiongeza kwamba "msaada wa taifa la Yemen kwa Gaza utaendelea kuongezeka kwa njia bora."

Tangu kuanza kwa vita vya mauaji ya kimbari vya Israel dhidi ya Gaza mnamo Oktoba 2023, Vikosi vya Jeshi la Yemen vimefanya oparesheni kadhaa kuwasaidia Wapalestina wa Gaza. Operesheni hizo zimelenga ngome za utawala haramu wa Israel, ikiwa ni pamoja na kushambulia meli za Israel au meli zinazokwenda kwenye bandari zinazokaliwa kwa mabavu na Israel.

Katika kuunga mkono Israel, Marekani ilitangaza kuunda kikosi cha majini katika Bahari ya Shamu mwezi Desemba 2023 ili kulinda meli zinazokwenda katika maeneo ya Palestina yanayokaliwa kwa mabavu na Israel. Jeshi la Yemen lilijibu hatua hiyo kwa kushambulia meli za kivita za Marekani katika Bahari ya Shamu. Jeshi la Marekani limepata hasara ya mamia ya mamilioni ya dola kutokana na mashambulizi ya Yemen. Katika kipindi cha wiki moja ndege mbili za kivita za Marekani aina ya F/A-18F Super Hornet zimeanguka katika Bahari ya Sham wakati zikitekeleza operesheni dhidi ya Yemen. Ndege moja ya F/A-18F Super Hornet inagharimu takribani dola milioni 66.

Rais Donald Trump alitangaza Jumanne kuwa Marekani itasitisha mashambulizi dhidi ya Yemen, akisema kuwa Yemen nayo imeafiki kusitisha kushambulia meli katika Bahari ya Shamu.

Baada ya tangazo la Trump, Oman imesema kuwa imefanikisha makubaliano ya kusitisha mapigano.

Msemaji wa Ansarullah amesisitiza kuwa kuwa pendekezo la Marekani la kusitisha mapigano lilionyesha udhaifu na kushindwa, kwani nchi hiyo ilishindwa kulinda meli za Israel.

Abdul-Salam amesisitiza kuwa Yemen bado inatathmini msimamo wa Marekani ili kuhakikisha kwamba sio tamko la maneno pekee.

Jumanne, Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman, Badr bin Hamad al-Busaidi, alisema, "Katika siku zijazo, hakuna upande utashambulia mwingine, ikiwemo meli za Marekani, katika Bahari ya Shamu na kifuatikizi cha Bab al-Mandab, kuhakikisha uhuru wa usafiri wa baharini na mtiririko wa usafirishaji wa kibiashara wa kimataifa."

Your Comment

You are replying to: .
captcha