Serikali ya mpito ya Israel imeunga mkono hatua inayozusha mabishano ya kuanzishwa wizara ziada.Baraza la mawaziri limeunga mkono mageuzi ya sheria ili kuzidisha idadi ya mawaziri,badala ya ile ya mawaziri 18 iliyokuwa ikitumika hadi sasa.Hata mawaziri wasiokuwa na wizara maalum watabidi kuteuliwa hivi sasa.Waziri mkuu Benjamin Netanyahu ameifanyia marekebisho kwa hivyo kanuni aliyoianzisha mwenyewe katika serikali iliyopita.Katika serikali mpya ,anahitaji idadi kubwa zaidi ya mawaziri,ili kuwaridhisha wafuasi wa chama chake cha Likud pamoja pia na wale wa vyama vinavyoshirikiana nae katika serikali ya muungano.Serikali hiyo iliyoundwa na vyama vitano kutoka mrengo wa kulia na kidini ina wingi wa kiti kimoja tu -viti 61 kati ya 120 vya bunge la Israel-Knesset.Bunge hilo litabidi liuidhinishe uamuzi wa serikali hadi kufikia jumatano ijayo.Na hadi wakati huo,serikali mpya inabidi iwe imeshaapishwa bungeni.Upande wa upinzani umeukosoa mpango wa kuzidisha idadi ya mawaziri wanaosema utagharimu mamilioni ya fedha.