Kundi la kigaidi la Daesh limedai linaudhibiti kikamilifu mji wa Ramadi magharibi ya Iraq. Katika taarifa iliyotolewa mapema leo kundi hilo limesema limeviteka vifaru na kuwaua wanajeshi kadhaa wa Iraq.
Kinyume na tangazo la kundi la kigaidi la Daesh, wizara ya ulinzi ya Marekani Pentagon imesema inaendelea kufuatilia ripoti za mapigano yanayoendelea mjini humo, huku ikikiri kuwa wanamgambo wa kundi hilo la kigaidi wanaonekana kuwa na nguvu zaidi katika makabiliano yanayoendelea. Msemaji wa wizara hiyo Maureen Schumann amesema ni mapema mno kutoa kauli kuthibitisha kinachoendelea katika mji wa Ramadi kwa sasa, lakini hata kama mji huo utaanguka mikononi mwa kundi la kigaidi la Daesh, muungano unaoongozwa na Marekani utawasaidia wanajeshi wa Iraq kuukomboa mji huo.
Wanajeshi wa Iraq walionekana wakiukimbia mji wa Ramadi wakiziacha silaha zao na magari yasiyoweza kutobolewa na risasi, katika kile kinachoonekana kuwa pigo kubwa la kushindwa vita dhidi ya magaidi wa Daesh licha ya ongezeko la mashambulizi ya kutokea angani dhidi ya kundi la kundi hilo la kigaidi linalodhaminiwa na Saudia arabia.
Maiti zilionekana zimezagaa katika barabara za mji huo, baadhi zikiwa zimechomwa moto, huku maafisa wakiripoti kwamba wanamgambo wa kundi hilo la kigaidi wamefanya mauaji ya halaiki dhidi ya wananchi wa Iraq.
Msemaji wa gavana wa mkoa wa Anbar Muhannad Haimour alisikika akisema"Mji wa Ramadi umeanguka. Mji umedhibitiwa kabisa na jeshi linakimbia,".
Kiongozi wa kiislamu wa dhehebu ya Sunni katika mji huo Naim al Guoud alisikika akisema: "Tunakaribisha kundi lolote, waje watusaidie kuukomboa mji wetu kutoka mikononi mwa magaidi wa Daesh. Kilichotokea leo ni hasara kubwa iliyosababishwa na jeshi kushindwa kujipanga vizuri,"
Gavana wa mkoa wa Anbar, Suhaib al Rawi, alisema anadhani harakati ya kijeshi inayofanywa na jeshi la Marekani ni hatua nzuri ya kuelekea kulishinda kundi la kigaidi la Daesh. "Operesheni yoyote ya maana inayofanywa na vikosi vya muungano dhidi ya kundi la kigaidi la Daesh itakuwa na matokeo mazuri. Kundi hili halitishii tu usalama wa Iraq na Syria bali pia usalama wa ulimwengu mzima. Tunahitaji operesheni za namna hii, zinazotoa ishara kwamba muungano wa kimataifa umejizatiti kuyashinda makundi ya kigaidi yanayotishia sio tu mkoa wa Anbar, Iraq na Syria bali dunia nzima."
Wakazi wa Ramadi wakimbia mji
Mamia ya wakazi wa Ramadi waliukimbia mji huo siku ya Jumamosi wakihofia mashambulizi ya wanamgambo wa kundi la kigaidi la Daesh lakini wakanyimwa ruhusa ya kuingia Baghdad na mikoa mingine na wanajeshi wa Iraq kwa sababu za kiusalama. Wakazi hao sasa wamekwama karibu na daraja la Bzibiz, kiasi kilometa 65 kutoka mji mkuu Baghdad na hawaruhusiwi kuvuka mto wa Euphrates kuelekea mji huo.
Um Mohammed, ambaye ni miongoni mwa wakaazi waliokwama, alisema hali ilikuwa ngumu Ramadi. "Vurugu, machafuko na hofu vimeenea katika barabara za Ramadi. Makombora na mabomu yalianguka kiholela kwa nyumba. Kuna ripoti mpya kwamba familia nyingi zimeuwawa. Wanawake walionekana wakikimbia mabarabarani."
Huku akikaribia kushindwa, waziri mkuu wa Iraq, Haider al-Abadi, aliamuru wanajeshi wasiondoke maeneo yao katika maeneo yote ya mkoa wa Anbar, akihofia wapiganaji wanaweza kuliteka eneo zima la jangwa lilishohudia mapigano makali baada ya uvamizi wa Iraq mnamo mwaka 2003 ulioongozwa na Marekani ambao ulimuangusha kiongozi wa zamani wa Iraq, hayati Saddam Hussein.
Marekani yafuatilia matukio ya Ramadi
Wizara ya ulinzi ya Marekani Pentagon imesema inaendelea kufuatilia ripoti za mapigano yanayoendelea mjini humo, huku ikikiri wanamgambo wa kundi hilo wanaonekana kuwa na nguvu zaidi katika makabiliano yanayoendelea. Msemaji wa wizara hiyo Maureen Schumann amesema ni mapema mno kutoa kauli kuthibitisha kinachoendelea Ramadi kwa sasa, lakini hata kama mji huo utaanguka mikononi mwa kundi la kigaidi la Daesh, muungano unaoongozwa na Marekani utawasaidia wanajeshi wa Iraq kuukomboa.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry alisema bado ana imani na vita dhidi ya kundi la kigaidi la Daesh. Akiwa katika ziara nchini Korea Kusini, Kerry amesisitiza vita dhidi ya kundi hilo vitakuwa vigumu na virefu katika mkoa wa Anbar, ambako wanajeshi wa Iraq hawajakuwa imara.
Jeshi la Shia ndio mkombozi pekee
Waziri mkuu wa Iraq, Haider al-Abadi ameomba kikosi cha kijeshi cha waislamu wa dhehebu la Shia kuingilia kati katika mapambano dhidi ya magaidi ya wa Daesh.
Kikosi cha jeshi la Shia ni kikosi maalum cha wananchi ambacho kimepata mafunzo kutoka kwa jeshi la Quds la Iran, kikosi hiki kinasifiwa kwa kuwa na nguvu na ustadi wa hali ya juu katika mapambano kuliko hata jeshi la Iraq.
Kikosi hiki ndicho kilichosababisha ushindi wa kuikomboa miji ya Tikrit na Salahudiin.
Kundi la kigaidi la Daesh linaonekana kuliogopa jeshi la mashia ambalo huwa halina sifa ya kukimbia wala vita.