Rais Vladimir Putin wa Urusi amesema nchi yake ilikuwa ikitoa mtizamo mbadala wakati ilipokuwa mwanachama wa nchi nane tajiri zaidi duniani zilizokuwa zikiunda G8 lakini nchi nyingine zenye nguvu zaidi duniani zilihisi hazihiitaji tena mtizamo wake. Putin ambaye yuko ziarani nchini Italia amesema Urusi haina uhusiano na kundi la G7 linalozishirikisha Ujerumani, Ufaransa, Italia, Canada, Japan, Marekani na Uingereza. Urusi iliondolewa kwenye kundi hilo la nchi tajiri zaidi duniani kutokana na kujiingiza katika mzozo wa Ukraine. Putin amesema utekelezwaji kamili wa makubaliano ya kusitisha mapigano ya Minsk ni muhimu katika kukomesha mapigano mashariki mwa Ukraine. Waziri mkuu wa Italia Matteo Renzi amemkaribisha Rais huyo wa Urusi kwa kuusifu urafiki alioutaja ni wa tangu jadi kati ya nchi hizo mbili lakini amezungumzia kuwepo tofauti fulani kutokana na mzozo wa Ukraine.