8 Agosti 2015 - 20:27
Waasi wauwa watu 12 nchini Mali

Watu 12 wameuwawa baada ya vikosi vya usalama nchini Mali kuivamia hoteli inayotumiwa na wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa na kuwakombowa mateka wanne waliokuwa wakishikiliwa na wanamgambo

Shirika la habari la ABNA linaripoti kuwa: Watu 12 wameuwawa baada ya vikosi vya usalama nchini Mali kuivamia hoteli inayotumiwa na wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa na kuwakombowa mateka wanne waliokuwa wakishikiliwa na wanamgambo.

Wanamgambo hao wa Kiislamu wa itikadi kali waliiteka hoteli ya Byblos ilioko katika mji wa Sevare kama kilomita 600 kaskazini mashariki ya mji mkuu wa nchi hiyo ya Afrika magharibi wa Bamako mapema Ijumaa na kuvizuwiya vikosi vya serikali vilivyowazingira visiikaribie hoteli hiyo.

Shambulio hilo ambalo limetokea mbali kabisa na eneo la kusini la jangwani ambayo ni ngome kuu ya wanamgambo wa Kiislamu wa itikadi kali kuanzia jadi ni la karibuni kabisa katika kile kinachoonekana kuwa kuongezeka kwa mashambulizi dhidi ya wanajeshi wa Mali na wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa yanayofanywa na mabaki ya waasi wenye mafungamano na kundi la kigaidi la Al Qaeda.

Msemaji wa wizara ya ulinzi ya Mali Kanali Diaran Kone amesema kuzingirwa kwa hoteli hiyo kumemalizika vizuri na kuwakombowa mateka wanne lakini kwa bahati mbaya pia wamegunduwa maiti tatu kwenye hoteli hiyo.

Msemaji wa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa nchini Mali MINUSMA amesema wafanyakazi wanne wa Umoja wa Mataifa wawili kutoka Afrika Kusini pamoja na Mrusi mmoja na Muukraine mmoja wamekombolewa katika shambulio lililofanywa na vikosi vya usalama kabla ya alfajiri.

Waliouawa katika tukio hili

Radhia Achouri amesema magaidi hawakuwahi kuwagunduwa wafanyakazi hao hotelini na kwamba wanachunguza iwapo kuna wafanyakazi wengine wa MINUSMA waliokuwepo kwenye hoteli hiyo.

Kwa mujibu wa msemaji wa serikali ya Mali Choguel Kokala Maiga mateka watatu waliuwawa wakati wa prukushani hiyo na wanatoka Afrika Kusini,Urusi na Ukraine.Wizara ya mambo ya nje ya Afrika Kusini imethibitisha kwamba raia wake wawili wako salama wakati mkaazi wa Pretoria mwenye umri wa miaka 38 aliyeajiriwa na kikosi cha MINUSMA kutoka kampuni ya masuala ya anga amefariki.

Amesema wanajeshi watano na wanamgambo wanne akiwemo yule ambaye awali ilisemekana alikuwa amevalia ukanda wa miripuko pia wameuwawa.

Awali Urusi na Ukraine zilithibitisha kwamba raia wake walikuwa miongoni mwa mateka waliokuwa wakishikiliwa kwenye hoteli hiyo.

Watuhumiwa saba mbaroni

Taarifa ya serikali iliyotolewa baadae hapo Ijumaa imesema watuhumiwa saba wamekamatwa kuhusiana na shambulio hilo.

Operesheni ya kijeshi ilioongozwa na Ufaransa hapo mwaka 2013 iliwatimuwa wapiganaji wa Kiislamu wa itikadi kali ambao walikuwa wametumia kwa faida yao uasi wa kabila la Tuareg na mapinduzi ya kijeshi kunyakuwa maeneo ya kaskazini mwaka mmoja kabla.

Wakati Umoja wa Mataifa umeweza kufankisha makubaliano dhaifu kati ya serikali na waasi wa Tuareg wanaotaka kujitenga wapiganaji wa Kiislamu wa itikadi kali ambao hawakujumuishwa kwenye mazungumzo hayo wamekuwa wakiendeleza harakati za uasi.

Hapo Ijumaa vikosi vya usalama vya Mali vilitumia silaha nzito yakiwemo maguruneti yanayovurumishwa kwa roketi kujaribu kuwachopowa bila ya mafanikio wanamgambo hao hotelini katika operesheni iliodumu kwa takriban saa 24.

Wanajeshi wa Ufaransa wanatajwa kukisaidia kikosi maalum cha Mali katika operesheni hiyo lakini jeshi la Ufaransa limesema halikuhusika moja kwa moja na kwamba dhima iliyotimiza ni ile ya uratibu ambayo ni ya kawaida kwa wakati huu.

Mwisho wa habari/ 291