Shirika la habari la ABNA linaripoti kuwa: Wanamgambo wanaojinasibisha na Uislamu wenye itikadi kali nchini Somalia wameishambulia hoteli moja mapema leo katika mji mkuu, Mogadishu, na kuwauwa karibu watu 12 na kuwajeruhi wengine zaidi ya kumi. Kapteni Mohamed Hussein amesema shambulizi hilo lilianza saa za alfajiri wakati mlipuaji wa kujitoa mhanga alipoliripua gari lililosheheni milipuko mlangoni mwa hoteli ya Sahafi na kisha watu waliokuwa na bunduki wakaingia ndani kwa miguu huku wakiwafyatulia watu risasi. Kulikuwa na mlipuko wa pili nje ya hoteli hiyo ambao unashukiwa kutoka kwenye bomu la kutegwa ndani ya gari lililokuwa limeegeshwa kando ya jengo hilo. Afisa huyo wa polisi amesema mmiliki wa hoteli hiyo, jenerali wa zamani wa jeshi na maafisa wengine ni miongoni mwa walioauwawa. Kundi la al-Shabaab limekiri kuhusika na shambulizi hilo.
Mwisho wa habari/ 291