8 Desemba 2020 - 12:07
Waziri wa Ulinzi wa Libya: Tutajitoa katika mapatano ya usitishaji vita iwapo Haftar atatekeleza shambulio la kijeshi

Waziri wa Ulinzi wa Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya amesisitiza kuwa, hawana chaguo jingine ghairi ya kudhibiti maeneo yote ya nchi hiyo. Aidha ametishia kuwa, serikali yao itajitoa kwenye mapatano ya kusitisha vita iwapo kutajiri mashambulizi kutoka upande wa Jenerali Khalifa Haftar.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Salahuddin al Namroush ameuomba Umoja wa Mataifa na nchi zinazosimamia mazungumzo kati ya pande za Libya kuchukua hatua za kusitisha hujuma za kijeshi za wanamgambo wanaoongozwa na Jenerali Khalifa Haftar. Baraza Kuu la Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa la Libya pia mapema jana lililaani shambulio lililofanywa na wanamgambo wa Haftar katika mji wa Awbari na eneo la kijeshi la Sabha kusini magharibi mwa Libya.  

Baraza hilo limetangaza katika taarifa yake kuwa, shambulio la wanamgambo wa Haftar na kitendo chao cha kupuuza mapatano ya usitishaji vita  vimejiri katika kutekeleza maagizo kutoka nje ya nchi; ambayo lengo lake ni kufelisha mwenendo wa kusaka amani nchini humo. 

Awbari ni mji wa pili kwa ukubwa huko Libya baada ya Sabha unaopatikana kusini mwa Libya. Katika mji huo kuna kisima cha mafuta cha Shararah ambacho ni mojawapo ya visima vikubwa zaidi vya mafuta nchini Libya. 

Waziri wa Ulinzi wa Libya amebainisha hayo katika hali ambayo pande zinazozozana nchini humo yaani Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa yenye makao huko Tripoli na kundi la Jeshi la Kitaifa linaloongozwa na Jenerali muasi Khalifa Haftar tarehe 23 mwezi Oktoba mwaka huu zilisaini huko Uswisi mapatano ya kusimamisha vita chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa. Mapatano hayo yalifikiwa baada ya mapigano ya miezi kadhaa kati ya pande mbili hizo. 

342/