30 Mei 2025 - 22:20
Source: Parstoday
Mkuu wa UNRWA: Waarabu wawape Wapalestina sehemu ndogo ya Matrilioni waliyompa Trump

Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa Linalowahudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) amezitaka nchi za Kiarabu katika Ghuba ya Uajemi kutenga sehemu ndogo tu ya fedha zilizotajwa katika ‘makubaliano makubwa’ kati yao na Rais wa Marekani, Donald Trump, ili kusaidia wakimbizi wa Kipalestina wanaopambana kuendelea kuishi katika ardhi zao ambazo Israel imezikalia kwa mabavu  na pia wale wanaoishi katika nchi jirani.

Philippe Lazzarini ameiambia tovuti ya Middle East Eye kwamba UNRWA, mtoaji mkubwa wa msaada kwa wakimbizi milioni sita wa Kipalestina, kwa sasa inakabiliwa na ‘upungufu wa fedha’ ambao huenda ukaibua maamuzi magumu.”

Ameongeza kuwa: “Kwa sababu ikiwa hatuna rasilimali, hatuwezi kuwalipa wafanyakazi. Huenda tukajikuta katika hali ambayo hata mishahara hatuwezi kuandaa. Na ikiwa hali hiyo itatokea, shirika litashurutika kuchambua ni huduma zipi kati ya huduma muhimu ni za dharura zaidi kuliko nyingine.”

Shirika la UNRWA, ambalo wafanyakazi wake wengi ni wakimbizi wa Kipalestina, limekuwa likilengwa na mashambulizi ya Israel tangu kuanza kwa vita vya mauaji ya kimbari dhidi ya Gaza mwezi Oktoba 2023. Takriban wafanyakazi wake 310 wameuawa na jeshi la Israel katika kipindi cha miezi 19 iliyopita, huku zaidi ya asilimia 80 ya majengo yake yakiharibiwa kabisa.

Lazzarini amezizihimiza nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi kuongeza ufadhili kwa UNRWA, akisema angependa kuona mikataba ya matrilioni ya dola waliyoingia na Trump katika ziara yake ya karibuni ikijumuisha pia msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina.

Katika ziara yake Asia Magharibi, Trump alitembelea Qatar, Saudi Arabia, na UAE, ambako mikataba yenye thamani ya zaidi ya dola bilioni 700 ilisainiwa. Ikulu ya Marekani ilitangaza kuwa jumla ya mikataba iliyokubaliwa ilikuwa dola trilioni mbili. Lazzarini amesema: “Natamani  hata tone tu la hizo trilioni zote za dola zilizotangazwa lingewafikia pia wakimbizi wa Kipalestina.”

Amesema kuwa hadi sasa, nchi za Kiarabu hazijatoa ufadhili wowote kwa UNRWA katika mwaka wa 2025. Ametoa wito kwa nchi za Kiarabu  kuwekeza katika shirika hilo sambamba na juhudi za kuunda taifa la Palestina lenye utawala kamili.

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha