Wawili hao wamezungumza kwa njia ya simu siku ya Alhamisi, wakitakiana heri ya Sikukuu ya Eid al-Adha, na kufungua ukurasa wa matumaini kwa mashauriano ya karibu zaidi ya kidiplomasia.
Katika mazungumzo hayo, Rais Pezeshkian alieleza utayari wa Tehran wa kupanua na kuimarisha uhusiano na Cairo katika nyanja zote, huku akitamani kukutana na mwenzake wa Misri mjini Tehran hivi karibuni kwa mazungumzo ya “kimaendeleo”.
Pezeshkian amesisitiza umuhimu wa kubadilishana tajriba, kutumia fursa za pamoja, na kushirikiana kwa nia ya kufanikisha maendeleo na ustawi wa mataifa ya Kiislamu. Ameyataka mataifa ya Kiislamu kuonesha mfano wa “undugu, mshikamano na ushirikiano wa kujenga”.
Akigusia mashambulizi ya kinyama ya Israel dhidi ya Wapalestina huko Gaza, Rais wa Iran alieleza haja ya kuwepo kwa mshikamano miongoni mwa mataifa ya Kiislamu ili kuchukua msimamo wa pamoja kukomesha ukatili wa Israel.
Kwa upande wake, Rais Sisi amebainisha hamu ya Misri ya kukuza uhusiano wa karibu zaidi na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Ameongeza kuwa anatumaini mataifa ya Kiislamu yatachukua hatua madhubuti katika kuimarisha amani, kukuza undugu na kupambana na maovu.
Ikumbukwe kuwa Israel ilianzisha kampeni ya mauaji ya kimbari dhidi ya watu wa Gaza mnamo Oktoba 7, 2023. Tangu wakati huo, zaidi ya Wapalestina 54,677 wameuawa.
Your Comment