Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Ayatollah Mohsen Faqihi, Mwanachama wa Jumuiya ya Walimu wa Hawza ya Qom, ametuma ujumbe wa shukrani kwa taifa tukufu la Iraq kwa mapokezi yao ya kipekee kwa mahujaji wa Arubaini ya Imam Hussein (a.s).
Katika ujumbe huu, Ayatollah Faqihi amesisitiza kuwa roho tukufu waliyonayo Wairaqi ni mwendelezo wa mwenendo wa Manabii na Mawalii, na ni ushahidi wa wazi juu ya utukufu wa taifa hili lenye heshima, ambalo kwa fahari na nguvu, limechukua jukumu la kuwa mabalozi wa ukarimu na ugeni.
Bismillahir Rahmanir Rahim
“Na anayeheshimisha alama za Mwenyezi Mungu, basi hakika hiyo ni katika unyenyekevu wa nyoyo.”
Enyi watu wapenzi wa Iraq, enyi wenye heshima, ukarimu na uaminifu kwa Ahlul-Bayt (a.s).
Amani, rehema na baraka za Mwenyezi Mungu ziwe juu yenu.
Kwa nyoyo zilizojaa shukrani na upendo, tunawapa heshima na pongezi kwa ugeni wenu wa kifakhari na mapokezi yenu bora katika siku hizi tukufu za Arubaini ya Imam Hussein (a.s). Nyinyi katika siku hizi mmeonyesha daraja za juu zaidi za ubinadamu na ujasiri, na mmekuwa wenyeji bora na waagizaji bora kwa mahujaji wa Bwana wetu, Sayyid al-Shuhadaa (a.s).
Mmeonyesha ulimwengu mzima kwamba imani ya kweli na mapenzi kwa Ahlul-Bayt (a.s) yamekita mizizi ndani ya nafsi zenu. Tumeona kwa macho yetu wenyewe namna mnavyojidhihirisha kwa kujitolea na kujisadikisha katika kuwatumikia mahujaji, na namna mlivyotoa kila kitu chenu ili kuhakikisha faraja na usalama wa kila mgeni aliyeelekea katika haram tukufu ya Imam Hussein (a.s). Msimamo huu wa fahari utabakia milele katika historia na ndani ya nyoyo za mamilioni ya wapenda Ahlul-Bayt (a.s).
Roho hii tukufu mliyo nayo ni mwendelezo wa mwenendo wa Manabii na Mawalii, na ni ushahidi thabiti juu ya utukufu wa taifa hili adhimu lililobeba bendera ya ugeni na ukarimu kwa fahari na taadhima.
Sasa tunainua mikono ya dua kwa Mola Mtukufu, tukimuomba akulindeni nyinyi na nchi yenu dhidi ya kila shari, azibariki jitihada zenu na aendelee kuwapeni neema ya amani na utulivu. Pia tunamuomba Mola awabariki wanazuoni wenu wakubwa, na hasa Marja’ mtukufu, Ayatollah al-Udhma Sayyid Ali al-Sistani (Mwenyezi Mungu adumishe kivuli chake kitukufu), ambaye kwa hekima na uongozi wake, Iraq inasonga mbele katika njia ya kheri na ukarimu.
Tunamuomba Mwenyezi Mungu akubali huduma zenu hizi tukufu, awape thawabu bora za watenda mema, na awakusanye pamoja na Mtume Muhammad (s.a.w.w) na kizazi chake kitukufu.
Amani na rehema za Mwenyezi Mungu ziwe juu yenu.
Hawza ya Qom
Mohsen Faqihi
21 Safar al-Muzaffar 1447
Your Comment