Pezeshkian alitoa kauli hiyo siku ya Jumamosi mjini Tehran, alipokutana na Katibu wa Baraza la Usalama la Armenia, Armen Grigoryan.
Katika mazungumzo hayo, aligusia makubaliano ya amani kati ya Armenia na Jamhuri ya Azerbaijan yaliyosimamiwa na Marekani, na kueleza wasiwasi kuhusu uwepo wa majeshi ya kigeni katika eneo hilo. Hata hivyo, alibainisha kuwa wasiwasi huo umepungua kwa kiasi kikubwa kufuatia maelezo na hakikisho kutoka kwa maafisa wa Armenia.
Mnamo Agosti 8, Armenia na Jamhuri ya Azerbaijan zilitiliana saini makubaliano ya amani mjini Washington, Marekani, ambapo walikubaliana kuanzisha njia ya usafiri itakayounganisha Jamhuri ya Azerbaijan na eneo lake la Nakhchivan, ambalo halina njia ya moja kwa moja ya kuunganishwa na maeneo mengine ya nchi hiyo.
Kupitia makubaliano hayo, Armenia ilikubali Marekani kuwa na haki ya kipekee ya kuendeleza njia hiyo katika mkoa wake wa kusini wa Syunik, unaopakana na Iran, ili kuwezesha muunganisho kati ya Azerbaijan na Nakhchivan.
Iran imekuwa ikipinga pendekezo hilo kwa muda mrefu, ikieleza kuwa litabadilisha mpangilio wa kijiografia wa eneo la Kusini mwa Kavkazia (Caucasus) na kupunguza uwezo wake wa kutumia mitandao ya usafiri katika ukanda huo.
Pezeshkian aliongeza kuwa katika ziara yake aliyoitaja kuwa yenye matunda nchini Armenia mwezi Agosti, viongozi wa ngazi ya juu kutoka pande zote mbili walifikia makubaliano chanya.
Aidha, alieleza kuridhika kwa Tehran kuhusu utekelezaji wa Mradi wa Njia ya Usafiri ya Kaskazini-Kusini, akisema kuwa kukamilika kwa mradi huo kutaimarisha mshikamano wa kiuchumi na kisiasa miongoni mwa wanachama wa Umoja wa Kiuchumi wa Eurasia.
Iran ni mshiriki wa Mradi wa Kimataifa wa Njia ya Usafiri ya Kaskazini-Kusini, mtandao wa takriban kilomita 7,200 unaojumuisha njia za meli, reli, na barabara, unaolenga kurahisisha usafirishaji wa mizigo kati ya Iran, Asia ya Kati, India, Jamhuri ya Azerbaijan, Urusi, na sehemu nyingine za Ulaya.
Kwa upande wake, Grigoryan alielezea ziara ya Pezeshkian nchini Armenia kuwa ya umuhimu mkubwa, na kupongeza juhudi zake za kuimarisha uhusiano wa pande mbili.
Alisema kuwa Tehran na Yerevan zina uhusiano wa kimkakati, na akaonesha utayari wa nchi yake kusaini hati ya ushirikiano wa kina. Afisa huyo wa juu wa usalama wa Armenia alionyesha matumaini kuwa miradi ya miundombinu na maendeleo nchini mwake itatekelezwa kwa kushirikiana na kampuni za Iran.
Your Comment