Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (a.s) -ABNA- Baraza hilo, katika taarifa yake, limewasilisha salamu za rambirambi kwa wananchi wa Afghanistan, hasa familia zilizoathirika, kufuatia janga hilo la kutisha.
Katika sehemu ya taarifa hiyo, wamenukuu aya tukufu ya Qur’ani isemayo:
"Na kwa yakini tutakujaribuni kwa kitu katika khofu, na njaa, na upungufu wa mali, na maisha, na mazao. Na wabashirie wanaosubiri."
(Qur’an 2:155)
Chombo hiki cha kidini na kijamii cha Waislamu wa Shia nchini Afghanistan, kimeeleza huzuni yake juu ya vifo na majeruhi ya idadi kubwa ya wananchi, pamoja na uharibifu wa makazi ya watu. Pia wameomba:
Rehema za Mwenyezi Mungu kwa waliopoteza maisha,
Uponyaji wa haraka kwa majeruhi,
Subira na uvumilivu kwa waliobaki.
Katika taarifa hiyo, imesisitizwa: “Msiba huu mkubwa, ukiwa sambamba na matatizo mengine ya hivi karibuni, unaugusa moyo wa kila mtu huru na mpenda nchi. Tunasimama pamoja na waathirika wote wa janga hili bila ya kujali kabila au madhehebu, na tunasisitiza juu ya mshikamano wa kitaifa na moyo wa undugu katika kupita kwenye kipindi hiki kigumu.”
Baraza hilo limezihimiza taasisi zote za misaada - za ndani na za kimataifa - kuhakikisha kuwa wanapeleka msaada wa haraka na wa kina kwa waathirika na kusaidia katika ujenzi upya wa maeneo yaliyoathirika vibaya.
Taarifa hiyo imemalizia kwa kuonyesha mshikamano wa dhati na kuwaombea watu wa Afghanistan heri na fanaka katika maisha ya dunia na akhera.
Kabul - (3 Septemba 2025).
Your Comment