
Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Sheikh Mkuu wa Jumuiya ya Shia Tanzania, Maulana Sheikh Hemed Jalala Mwakindenge, ameungana na waumini na viongozi mbalimbali wa dini katika hafla maalumu ya ndoa za vijana 100, iliyoandaliwa kama sehemu ya maadhimisho ya mazazi yenye baraka ya Bibi Fatima Zahra (s.a).

Hafla hiyo ambayo imekuwa desturi kufanyika kila mwaka katika siku hizi tukufu, imehudhuriwa na Masheikh na wageni mashuhuri kutoka maeneo mbalimbali ya nchi, wakiongozwa na Mgeni Rasmi, Sheikh wa Mkoa wa Tanga Ali Juma Luwuchu.

Katika hotuba yake, Sheikh Jalala Mwakindenge amesisitiza umuhimu wa kujenga familia imara zenye misingi ya Qur’ani na Sunna, sambamba na kutangaza furaha katika masiku ya watu wa Nyumba ya Mtume (a.s). Aidha amewapongeza vijana waliofunga ndoa na kuwahimiza kuishi kwa mapenzi, heshima na uaminifu.

Viongozi wengine waliohudhuria pia wameisifu juhudi hii yenye lengo la kuwawezesha vijana kuanza maisha ya ndoa kwa utulivu, huku wakisisitiza kuendelea kuenzi mafunzo ya Bibi Fatima Zahra (a.s) katika ujenzi wa jamii yenye maadili mema.

Hafla hii imeendelea kuwa ishara ya umoja, upendo na kuenzi Sunna ya ndoa katika Uislamu, sambamba na kuadhimisha tukio tukufu la mazazi ya Bibi Fatima Zahra (s.a).

Your Comment