31 Agosti 2025 - 08:41
Source: Parstoday
Larijani: Iran inapinga mabadiliko ya kijiografia katika ukanda wa Kavkazia

Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran, Ali Larijani, ameeleza kuwa Tehran inapinga vikali hatua yoyote inayoweza kuathiri muundo wa kisiasa na kijiografia wa eneo la Kavkazi (Caucasus)

Akizungumza  katika mkutano na mwenzake kutoka Armenia, Armen Grigoryan, Larijani amepongeza ushiriki wa Armenia katika njia kuu ya usafirishaji inayopita ndani ya Iran, ikiziunganisha nchi za kaskazini na Bahari ya Oman.

Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika jijini Tehran Jumamosi, Larijani ameonyesha kuridhishwa na kiwango cha ushirikiano wa kiuchumi, kisiasa, kiusalama na kijeshi kati ya Iran na Armenia. Amesisitiza umuhimu wa kukamilisha Mradi wa Njia ya Usafirishaji ya Kaskazini-Kusini, ambao unahusisha mtandao wa kimataifa wa usafirishaji wa mizigo kupitia meli, reli na barabara, unaounganisha Iran na mataifa ya Asia ya Kati, India, Jamhuri ya Azerbaijan, Russia na Ulaya.

Kupitia Iran kama kitovu cha usafirishaji, nchi zisizo na bandari katika Asia ya Kati zitapata fursa ya kuunganishwa na mtandao wa kimataifa wa biashara na usafirishaji. Larijani pia ametangaza uungaji mkono wa Iran kwa mazungumzo ya amani kati ya Armenia na Jamhuri ya Azerbaijan, akieleza kuwa Iran daima imekuwa ikitetea uhuru na uimara wa mataifa ya ukanda huu kama njia ya kuhakikisha usalama wa kudumu.

Kwa upande wake, Armen Grigoryan amepongeza uhusiano wa pande mbili kati ya Armenia na Iran, akieleza kuwa ziara yake inalenga kuimarisha ushirikiano katika nyanja mbalimbali. Amesema kuwa Armenia inatarajia kusaini hati ya ushirikiano wa kimkakati na Iran katika siku za usoni.

Grigoryan amesisitiza kuwa nchi yake inatilia mkazo kanuni za uhuru wa kitaifa, heshima kwa mipaka ya kitaifa, mamlaka ya kisheria ya kitaifa, kutovunjika kwa mipaka, na usawa wa pande mbili. Ameongeza kuwa Yerevan iko tayari kutoa dhamana kwa Tehran kuhakikisha kuwa uhusiano kati ya mataifa hayo mawili hauathiriki.

Katika muktadha wa mazungumzo ya amani na Jamhuri ya Azerbaijan, Grigoryan amebainisha kuwa makubaliano yaliyofikiwa yamehifadhi kwa uwazi mamlaka ya Armenia katika masuala ya usalama, kijeshi na forodha. Na kwa mara nyingine, amesisitiza msimamo wa Armenia wa kupinga mabadiliko ya kijiografia katika ukanda huo wa Kavkazia.

Your Comment

You are replying to: .
captcha