Baada ya kikao hicho, Amir Saeid Iravani, Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa alikosoa hatua "isiyo ya kisheria" ya nchi tatu za Ulaya (Uingereza, Ufaransa na Ujerumani) ya kutangaza kuanza mchakato wa kurejesha vikwazo vya Baraza la Usalama dhidi ya Iran na kusema kuwa, hatua hiyo imetupilia mbali utaratibu wa utatuzi wa mizozo wa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na kuongeza kuwa: "Iran imejitolea kufuata njia ya diplomasia, lakini kamwe haitafanya mazungumzo chini ya vitisho au kwa kulazimishwa." Iravani amesema, hatua ya Troika ya Ulaya imechukuliwa kwa shabaha ya kuitisha Iran na kuiwekea mashinikizo ya kisiasa. Kwa mujibu wa balozi wa kudumu wa Iran UN, ombi la kufanyika kikao cha faragha cha Baraza la Usalama la Ufaransa na Uingereza pia lilitolewa ili kuhalalisha hatua hiyo isiyo ya kisheria na kwa malengo ya kisiasa na kulitumia Baraza la Usalama la UN kama chombo cha kutimiza malengo yao na dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.
Troika ya Ulaya imecheza turufu yake ya mwisho dhidi ya Iran?
Iran imetoa sababu kadhaa za kupinga hatua ya nchi za Ulaya ya kutekeleza mchakato wa snapback. Azimio nambari 2231, lililoidhinisha makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, lilitoa fursa ya snapback kwa wanachama walioshiriki katika makubaliano hayo, lakini kivitendo, Wazungu hawajachukua hatua yoyote madhubuti kulinda JCPOA. Iran inatoa hoja kwamba, nchi za Ulaya haziwezi kutumia chombo hicho isipokuwa chini ya masharti maalumu yaliyoainishwa katika maandishi ya makubaliano hayo, na masharti hayo bado hayajatimia. Iran pia inaamini kwamba, kwa kutishia kuanza mchakato wa kurejesha vikwazo vya Baraza la Usalama dhidi ya Tehran na sasa kuanza kuutekeleza, nchi za Ulaya kwa hakika zinatumia makubaliano ya kimataifa kama chombo cha mashinikizo ya kisiasa na sio kudumisha amani na usalama. Kwa mtazamo wa Iran, hatua hizo za Ulaya zinadhoofisha mchakato wa diplomasia na mazungumzo na kuharibu hali ya kuaminiana baina ya pande zote.
Jambo la kuashiria ni kwamba, Ijumaa, Agosti 29, balozi wa Uingereza katika Umoja wa Mataifa, anayewakilisha Troika ya Ulaya, alihalalisha hatua ya nchi yake dhidi ya Iran na kudai kwamba kipindi cha siku 30 cha kuaanza kutekelezwa mchakato wa kurejeshwa vikwazo vya UN dhidi ya Iran hakina maana ya mwisho wa diplomasia. Amedai kuwa: "Mapendekezo yetu bado yako mezani na tunaendelea kushikamana na diplomasia na tunaihamasisha Iran ikubaliane na pekezo letu."
Nchi tatu za Ulaya ambazo ni wanachama wa kundi la 4+1, ikiwa ni pamoja na Ujerumani, Ufaransa na Uingereza, zinazojulikana kama Troika ya Ulaya, ambazo bado hazijatekeleza majukumu yao chini ya makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, zilituma "taarifa" katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa siku ya Alhamisi, Agosti 28, 2025, zikitaka kuanza kutekelezwa mchakato kurejesha vikwazo vya Baraza la Usalama dhidi ya Iran (snapback). Nchi hizo zilitangaza masharti kadhaa na kusema ziko tayari kufanya mazungumzo na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika muda wa siku 30 zijazo kuhusu makubaliano ya nyuklia yanayoweza kusimamisha mchakato wa kurejeshwa vikwazo.
Kinachostahili kuzingatiwa hapa ni tofauti ya wazi katika msimamo wa nchi tatu zenye nguvu za Magharibi na Mashariki, ambazo ni Marekani dhidi ya Russia na Uchina, kuhusu kuanza kwa mchakato wa snapback uliopendekezwa na Troika ya Ulaya. Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, amekaribisha hatua hiyo ya Troika ya Ulaya na kutangaza kwamba: "Katika wiki zijazo, tutashirikiana na Troika ya Ulaya na wajumbe wengine wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ili kukamilisha kwa mafanikio mchakato wa kurejesha vikwazo vya kimataifa dhidi ya Iran, kwa mujibu wa agizo la Rais wa Marekani."
Marco Rubio
Mkabala wake, Russia na China zimekosoa hatua ya Troika ya Ulaya na kuitaja kuwa sio halali. Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia imekumbusha kwamba Iran imekuwa ikitekeleza mapatano ya JCPOA kwa uaminifu kwa miaka kadhaa, na kuitaja hatua ya Troika ya Ulaya ya kurejesha vikwazo vya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran (snapback) kuwa ni kinyume na sheria. Russia pia imelaani kitendo hicho. Wizara ya Mambo ya Nje ya China pia imesema kuwa, kuwekwa tena vikwazo dhidi ya Iran katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ni hatua isiyofaa na kusisitiza kuwa: Faili la nyuklia la Iran liko katika hatua muhimu na mazungumzo lazima yaanzishwe tena.
Miongoni mwa nukta muhimu za kuashiria ni kwamba, hata duru za nchi za Magharibi zina shaka kubwa kuhusu ufanisi wa hatua ya Troika ya Ulaya dhidi ya Iran. Taasisi ya Quincy Institute ya Marekani imeandika katika makala iliyopewa jina la "Kamari ya Wazungu Kuhusu Utekelezaji wa Snapback Unahatarisha Kuharibu Diplomasia na Iran", kwamba: Iwapo Ulaya inafadhilisha njia ya kutwisha na kulazimisha badala ya ushirikiano, dirisha la fursa iliyopo linaweza kufungwa kabisa."
Jarida la Foreign Policy pia limeelezea shaka yake kuhusu mafanikio ya kutekelezwa mchakato wa snapback na kuandika: "Kurejeshwa vikwazo vya Baraza la Usalama dhidi ya Iran ni hatua ya kinembo zaidi na hakuwezi kuilenga Iran; na Russia na China pia zinaweza kuvuruga utekelezaji wa vikwazo hivyo."
Your Comment