Kupitia barua rasmi kwa Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya, Bi Kaja Kallas, anayeratibu Tume ya Pamoja ya Makubaliano ya Nyuklia ya JCPOA, Araghchi amesisitiza kuwa Azimio 2231 “linapaswa kumalizika kulingana na ratiba yake rasmi mnamo Oktoba 18, 2025.”
Amesema: “Juhudi za nchi hizo tatu za Ulaya (E3) kufufua maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa yaliyofutwa chini ya Azimio 2231 ni batili na hazina athari yoyote.”
Barua ya Araghchi imewasilishwa siku moja baada ya E3 kuanzisha utaratibu wa kurejesha vikwazo (snapback), hatua inayofungua dirisha la siku 30 kwa uwezekano wa kurejesha vikwazo dhidi ya Tehran.
Araghchi amesisitiza kuwa viongozi wa Ulaya hawana “mamlaka ya kisheria ya kuanzisha urejeshaji wa moja kwa moja wa vikwazo,” akisema kuwa hatua yao inapuuza “ukweli muhimu na historia ya mchakato wa makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015.”
Amekumbusha kuwa miongoni mwa nchi zilizotia saini mapatano ya nyuklia ya JCPOA, Iran ndiyo iliyokuwa ya kwanza kuanzisha utaratibu wa utatuzi wa mgogoro baada ya Marekani kujiondoa mwaka 2018.
Akiashiria kushindwa kwa mataifa ya Ulaya kutekeleza “ahadi 11 za ziada” zilizolenga kulinda makubaliano ya JCPOA, Araghchi amekosoa mfumo wa kifedha wa Umoja wa Ulaya, INSTEX, akisema ni “wa kimaonyesho tu na haukuwa na ufanisi.” Mfumo huo ulilenga kutatua matatizo ya mabadilishano ya kifedha ya Iran baada ya Marekani kujiondoa katika JCPOA.
Amesema kuvunjika kwa mazungumzo ya hivi karibuni mjini Vienna kulitokana na “msimamo wa ukaidi wa Marekani, vikwazo vya kisiasa vya ndani na sisitizo la E3 la kuhusisha mazungumzo na masuala yasiyoendana.”
Araghchi pia amelaani kimya cha Umoja wa Ulaya kuhusu mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya vituo vya nyuklia vya Iran mwezi Juni, akisema kimya hicho ni “ukiukaji wa wazi wa Hati ya Umoja wa Mataifa na sheria za kimataifa,” na akakosoa uungaji mkono wa Ulaya kwa hatua hizo za kichokozi.
Akisisitiza utayari wa Iran kuendelea na mazungumzo ya kidiplomasia yenye usawa na haki, Araghchi amehimiza Umoja wa Ulaya kuepuka “tafsiri za upande mmoja” na kuendeleza “diplomasia ya kweli na kulinda mfumo wa ushirikiano wa kimataifa.”
Barua hiyo pia imetumwa kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, pamoja na wajumbe wote wa Baraza la Usalama.
Araghchi amewahimiza wajumbe hao “kukataa njama za kisiasa zisizo na msingi na kulinda uadilifu wa sheria za kimataifa pamoja na mamlaka ya Baraza hilo.”
Your Comment