Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari akiwa pamoja na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron mjini Toulon, Merz amesema, licha ya matumaini yaliyojitokeza baada ya juhudi za kidiplomasia za Rais wa Marekani Donald Trump, mkutano wa viongozi wa Russia na Ukraine unaelekea kuwa hautawezekana kufanyika.
"Ni wazi hakuna nia ya Rais Putin kukutana na Rais Zelenskyy. Anaweka masharti ambayo hayakubaliki," ameeleza Kansela wa Ujerumani na kuongezea kwa kusema: "kusema ukweli, hii hainishangazi, kwa sababu ni sehemu ya mkakati wa rais wa Russia".
Kiongozi huyo wa kihafidhina amesema Marekani na washirika wake wa Ulaya wanapaswa wiki ijayo kujadili kwa makini hatua zinazowezekana kutekelezwa ili kuongeza mashinikizo kwa Russia, na kuilazimisha ishiriki kwenye diplomasia na Ukraine na kukubali usitishaji mapigano.
Pamoja na hayo, Merz amesisitiza kwa kusema: "hata hivyo, siliangalii hilo pia kidhahania. Vita hivi vinaweza kudumu kwa miezi mingi zaidi. Tunapaswa kuwa tayari kwa hilo kwa vyovyote vile. Tunajiandaa kwa hilo kwa uratibu wa karibu na washirika wetu wa Ulaya, na Wamarekani, na pia na muungano wa watakaojitolea".../
Your Comment