3 Septemba 2025 - 00:15
Source: Parstoday
Iran, Russia kuimarisha uhusiano wao kupitia mikataba ya muda mrefu

Rais Masoud Pezeshkian wa Iran, na mwenzake wa Russia, Vladimir Putin wamesisitiza umuhimu wa kutekelezwa Mkataba Kamili wa Ushirikiano wa Kistratejia kati ya nchi mbili hizo.

Marais hao wawili walitoa mwito huo walipokutana pambizoni mwa mkutano wa 25 wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Shanghai (SCO) huko Tianjin nchini China, jana Jumatatu. Rais Pezeshkian ameutaja mkataba huo wa Russia na Iran kama msingi wa kupanua ushirikiano na kuimarisha uhusiano wa pande mbili.

Amebainisha kuwa, ushirikiano ndani ya mfumo wa Umoja wa Kiuchumi wa Eurasia (EAEU) utaongeza kasi zaidi na kukuza maendeleo haya. Rais wa Iran amesisitiza dhamira yake binafsi ya kuondoa vizingiti na kuharakisha utekelezaji wa makubaliano yote na Russia.

Hali kadhalika, Rais wa Iran amesisitiza umuhimu wa kubadilishana mawazo katika nyuga za sayansi na kitaaluma, akibainisha kuwa ushirikiano huo utajenga jukwaa la mwingiliano mpana na wa pande nyingi.

Pezeshkian ameashiria mkutano wa kilele wa SCO, akisisitiza jukumu la taasisi za kimataifa kama jumuiya hiyo ya Shanghai katika kuendeleza ushirikiano wa kimataifa katika kukabiliana na jitihada za Marekani na washirika wake za kuimarisha hatua za upande mmoja.

Rais Putin kwa upande wake ametuma salamu na kumtakia kheri Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, na kusisitiza kwamba uhusiano kati ya Iran na Russia ni wa kirafiki na unazidi kuimarika siku baada ya siku.

Rais wa Russia amesema anaridhishwa na ongezeko kubwa la biashara baina ya nchi hizo mbili, kuogezeka idadi ya wanafunzi wa Iran wanaosoma nchini Russia, na kupanuka kwa ushirikiano wa kitamaduni na utalii baina ya nchi mbili. 

Your Comment

You are replying to: .
captcha