Pezeshkian aliyasema hayo jana Jumatatu katika hotuba yake kwenye Mkutano wa 'Shanghai Plus' kwenye mji wa bandari wa Tianjin nchini China, uliofanyika baada ya Mkutano wa 25 wa Baraza la Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Ushirikiano wa Shanghai (SCO).
Akiashiria vitendo vya uchokozi vya Israel na Marekani dhidi ya Iran mwezi Juni, wakati ambapo Washington ilikuwa ikifanya mazungumzo na Tehran "kinafiki", amesema mashambulio hayo yalithibitisha kuwa chaguo la kijeshi haliwezi kufaulu, na litakabiliwa na Muqawama wa kishujaa wa wananchi wa Iran.
Rais wa Iran ameonya kwamba, hatua ya Ulaya ya kutumia kile kinachoitwa utaratibu wa kuiwekea vikwazo Iran "itafanya hali kuwa ngumu zaidi na kusababisha mvutano zaidi." Ametoa wito kwa jumuiya ya SCO na nchi huru duniani kuchukua jukumu madhubuti na la uwajibikikaji, mbele ya hatua hizo zisizo za haki.
Dakta Pezeshkian kwa mara nyingine tena amethibitisha utayarifu wa Jamhuri ya Kiislamu wa kutafuta suluhu ya kidiplomasia kwa njia ya amani, kwa masuala yanayohusu mpango wake wa nishati ya nyuklia.
Kwingineko katika hotuba yake, Rais wa Iran ameitaka SCO, kama moja ya vyombo muhimu vya kujitegemea na vya kutafuta haki duniani, kuweka mikakati kabambe ya kukuza amani ya kimataifa.
Your Comment