3 Septemba 2025 - 00:16
Source: Parstoday
Jenerali Mousavi: ‘Kinara wa Magaidi’ Israel inaogopa kupanuka kwa Mhimili wa Muqawama

Kamanda mwandamizi wa Jeshi la Iran amelaani vikali mauaji ya hivi karibuni ya maafisa wa juu wa Yemen, yaliyotekelezwa na utawala wa Israel, akiyataja kama ishara ya hofu kubwa ya Tel Aviv kuhusu kuongezeka kwa nguvu za Mhimili wa Muqawama katika eneo la Asia Magharibi.

Meja Jenerali Abdolrahim Mousavi, Mkuu wa Kamandi ya Majeshi ya Iran, alitoa kauli hiyo siku ya Jumatatu kupitia ujumbe rasmi kwa taifa la Yemen kufuatia mashambulizi hayo ya anga.

"Uhalifu huu unadhihirisha hofu kubwa ya utawala wa Israel kuhusu kupanuka Mhimili wa Muqawama," alisema kwa msisitizo.

Aidha, Jenerali Mousavi aliongeza kuwa utawala huo unaogopa umoja unaozidi kuimarika miongoni mwa mataifa ya kanda hii katika harakati za kulitetea taifa la Palestina, linalopigania kujikomboa kutoka kwenye uvamizi na unyanyasaji wa Israel.

Akiendelea kulaani mashambulizi hayo, Mousavi aliyataja kuwa ni "uhalifu mkubwa wa kivita, shambulio la kigaidi, na ukiukwaji wa wazi wa sheria za kimataifa." Amesema vitendo hivyo ni fedheha nyingine kwa utawala wa Israel, ambao ameuita "kinara wa ugaidi na mlezi wa magaidi duniani."

Kwa mujibu wa Jenerali Mousavi, mauaji hayo yanatekelezwa kwa kuzingatia sera ya muda mrefu ya ukandamizaji, unyakuzi wa ardhi, na mashinikizo ya waitifaki wa Israel, hususan Marekani.

Ujumbe huo umetolewa baada ya mashambulizi ya anga ya Israel dhidi ya mji mkuu wa Yemen, Sana’a, ambapo miongoni mwa waliouawa shahidi ni Waziri Mkuu Ahmed Ghaleb al-Rahawi pamoja na mawaziri kadhaa.

Mashambulizi haya yanajiri katika muktadha wa hujuma za mara kwa mara za utawala huo dhidi ya Yemen, ambazo zilianza baada ya Jeshi la Yemen kuanzisha operesheni karibu kila siku dhidi ya malengo nyeti ya Israel. Hatua hiyo ni jibu kwa vita vya mauaji ya kimbari vilivyoanzishwa na Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza mnamo Oktoba 2023.

Jenerali Mousavi amesisitiza kuwa vitendo vya kinyama kama hivyo "havitavunja moyo wala kutishia dhamira ya mapinduzi na azma ya wapiganaji jasiri wa Yemen."

Amehitimisha kwa kusema kuwa Yemen, kupitia mapambano yake ya kudumu, imekuwa nembo ya upinzani dhidi ya mfumo wa kimataifa wa kibeberu, na chanzo cha fahari kwa umma wa Kiislamu duniani. Iran, amesema, itaendelea kutoa msaada kwa watu wa Yemen katika harakati zao za kujikomboa.

Your Comment

You are replying to: .
captcha