3 Septemba 2025 - 00:20
Source: Parstoday
Maduro: Tutaitangaza Venezuela 'jamhuri yenye silaha' ikiwa US itatushambulia

Rais wa Venezuela, Nicolas Maduro amesema kuongezeka uwepo wa majeshi ya Marekani katika eneo la Caribbean kunalenga kuipindua serikali yake, na kusisitiza kuwa yuko tayari "kutangaza jamhuri yenye silaha" ikiwa nchi hiyo itashambuliwa na wanajeshi hao wavamizi.

Katika matamshi adimu mbele ya waandishi wa habari jana Jumatatu, Maduro amesema kuwa Venezuela inataka amani, lakini jeshi lake liko tayari na limejiandaa barabara kujibu mashambulizi yoyote kutoka kwa vikosi vya Marekani.

"Wanafuatilia kupindua serikali kupitia vitisho vya kijeshi," Maduro amewaambia waandishi wa habari na kueleza bayana kuwa, "Venezuela inakabiliwa na tishio kubwa zaidi ambalo halijawahi kushuhudiwa katika bara letu katika miaka 100 iliyopita."

"Ikiwa Venezuela itashambuliwa, tutageukia mara moja kwenye mapambano ya silaha kupigania ardhi yetu," amesema akiapa kutangaza "jamhuri yenye silaha".

"Katika kukabiliana na mashinikizo haya ya juu ya kijeshi, tumetangaza kujiandaa kwa kiwango cha juu kwa ulinzi wa Venezuela", Maduro amefafanua zaidi na kudokeza kwamba, Marekani tayari imetuma "meli nane za kijeshi zilisheheni makombora 1,200 na nyambizi kwa ajili ya kuishambulia Venezuela".

Venezuela tayari imetangaza kuwa imepeleka meli za kivita na ndege zisizo na rubani kwenye eneo lake la maji na kufanya doria kwenye ufuo wa pwani ya nchi hiyo, ili kukabiliana na hatua ya Marekani ya kutuma meli kadhaa za kivita katika eneo la Caribbean kwa kile ilichodai ni kwa ajili ya kukabiliana na biashara ya mihadarati na kumshinikiza Rais Nicolás Maduro.

Waziri wa Ulinzi wa Venezuela, Vladimir Padrino, alitngaza hivi karibuni kwamba, "doria za majini zimetumwa kwenye Ghuba ya Venezuela na pwani ya Caribbean, meli kubwa kaskazini mwa eneo letu la maji," pamoja na "idadi kubwa ya ndege zisizo na rubani."

Your Comment

You are replying to: .
captcha