3 Septemba 2025 - 23:37
Source: Parstoday
Chuo Kikuu cha Utrecht ni cha kwanza Magharibi kususia Israel kwa sababu ya mauaji ya kimbari Gaza

Chuo Kikuu cha Utrecht cha Uholanzi kimekuwa taasisi ya kwanza ya kielimu katika nchi za Magharibi kuususia kikamilifu utawala dhalimu wa Israel kufuatia mauaji ya kimbari yanayoendelezwa na utawala huo huko Gaza.

Hatua hii inawakilisha tukio la kihistoria linalovunja mwiko wa zamani uliokuwepo katika jamii za kitaaluma za Magharibi. Uamuzi huo, ulioidhinishwa kupitia taarifa ya Mkuu wa Chuo, Wilco Hazeleger, umetolewa baada ya shinikizo la muda mrefu kutoka kwa wanafunzi na wafanyakazi waliokuwa wakifanya maandamano.

Chuo hicho kimesitisha ushirikiano wote wa kimataifa na taasisi za Israel na hakitaanzisha ushirikiano wowote mpya, huku zuio hilo likidumu hadi taarifa nyingine itakapotolewa. Hazeleger ameeleza kuwa hatua hiyo ni ya lazima kimaadili. “Hali ya dunia, hasa ya Gaza, inatulazimu tuchukue msimamo wa kimaadili. Kuna mateso makubwa ya kibinadamu,” amesema.

Ingawa amesisitiza wajibu wa taasisi za kitaaluma kuhamasisha majadiliano ya wazi na utafiti wa amani, ameongeza kuwa mstari wa maadili umekiukwa. “Ni wazi kuwa kuna ukatili wa kimbari na mstari huo umevukwa.” Hatua hii inaendana na malengo ya Kampeni ya Palestina ya Kususia Israel Kitaaluma na Kiutamaduni (PACBI), ambayo ni matokeo ya juhudi za kimkakati za wanafunzi na wafanyakazi wa vyuo vikuu. Zuio hili linakuja wakati ambapo kuna upinzani mkubwa wa kimataifa dhidi ya vita vya mauaji ya kimbari vinavyoendeshwa na Israel dhidi ya Gaza na uvamizi wa muda mrefu wa ardhi za Wapalestina.

Duniani kote, jamii za kitaaluma na wanafunzi wameongeza mashinikizo dhidi taasisi zao ili kupiga marufuku ushirikiano na vyombo vya Israel vinavyohusika moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja katika kuhalalisha ubaguzi wa rangi, utafiti wa kijeshi au kudumisha uvamizi dhidi ya Wpalestina.

Utawala wa Israel ulianzisha mashambulizi makubwa dhidi ya Gaza tarehe 7 Oktoba 2023, baada ya wapiganaji wa Muqawama wa Kipalestina kuendesha Operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa, wakijibu kampeni ya muda mrefu ya mauaji na uharibifu ya utawala huo dhidi ya Wapalestina. Kulingana na Wizara ya Afya ya Gaza, Wapalestina wasiopungua 63,633 wameuawa na zaidi ya 160,914 kujeruhiwa tangu kuanza kwa vita hivyo, wengi wakiwa ni wanawake na Watoto.

Your Comment

You are replying to: .
captcha