3 Septemba 2025 - 23:39
Source: Parstoday
IRIB yalaani mauaji ya mwanahabari wa Al-Alam huko Gaza

Kitengo cha Kimataifa cha Shirika la Utangazaji wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran IRIB kimelaani vikali mauaji ya Rasmi Jihad Salem, mpigapicha wa kanali yake ya Kiarabu ya Al-Alam, ambaye aliuawa shahidi katika shambulio la Israel huko Gaza jana Jumanne, Septemba 2 alipokuwa akirejea kutoka kazini.

IRIB imesema Salem alikuwa akirekodi na kunakili "uhalifu dhidi ya watu wa Palestina" wakati alipouawa shahidi, na kusisitiza kuwa utawala wa Kizayuni unajaribu kunyamazisha sauti zinazofichua ukweli wa mambo huko Gaza.

Taarifa ya Kitengo cha Kimataifa cha IRIB imesema kuwa, "Uhalifu huu unaongeza rekodi ndefu ya jinai za utawala wa Kizayuni. Vikosi vamizi sio tu vinaua wanawake na watoto bali pia huwanyamazisha wasema ukweli kwa kutumia risasi."

Taarifa hiyo imemsifu Salem na kumueleza kama "mwandishi wa habari aliyejitolea muhanga, na ambaye aligeuza kamera yake kuwa ngome, na picha zake kuwa ushuhuda."

Haya yanajiri huku mashambulizi ya jeshi la Israel dhidi ya Jiji la Gaza yakiendelea bila kukoma, na kusababisha mauaji ya makumi ya Wapalestina, wakiwemo 32 waliokuwa wakitafuta misaada. Takriban Wapalestina 105 wakiwemo wanahabari waliuawa shahidi katika eneo lote la Gaza jana Jumanne, wakati mashambulio ya Israel yakilenga maeneo yenye watu wengi, hasa kitongoji cha al-Sabra, ambacho kimekuwa kikishambuliwa kwa siku kadhaa. 

Juzi Jumatatu, mwandishi wa Televisheni ya Al-Quds Today aliuawa shahidi katika shambulizi la Israel huko Gaza na hivyo kuzidisha idadi ya waandishi wa habari waliouawa shahidi katika vita na mauaji ya kimbari yanayotekelezwa na Israel katika Ukanda wa Gaza.

Waandishi wa habari zaidi ya 200 wameuawa shahidi na jeshi katili la Israel tangu utawala huo ghasibu uanzishe vita na mauaji ya kimbari dhidi ya wakazi wa Gaza Oktoba 7, 2023. 

Your Comment

You are replying to: .
captcha