15 Septemba 2025 - 23:38
Source: Parstoday
WHO: Vifo vilivyosababishwa na kipindupindu duniani kote katika mwaka 2024 viliongezeka kwa 50%

Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza kuwa vifo vilivyosababishwa na ugonjwa wa kipindupindu viliongezeka kwa asilimia 50 duniani kote katika mwaka uliopita wa 2024 ikilinganishwa na mwaka wa kabla yake.

Takwimu za WHO zimeonyesha pia kuwa kesi zilizoripotiwa za ugonjwa huo ziliongezeka kwa asilimia tano.

Kwa mujibu wa shirika la afya duniani, karibu kesi za maambukizo 560,000 ziliripotiwa katika nchi na maeneo 60 duniani. Aidha, zaidi ya watu 6,000 walikufa kutokana na ugonjwa huo. Mnamo mwaka 2023, ugonjwa wa kipindupindu uliripotiwa katika nchi na maeneo 45 tu.

Imeelezwa kwamba, kesi nyingi za ugonjwa huo zilikuwa barani Afrika, Mashariki ya Kati na Asia, ambazo kwa pamoja zilichangia asilimia 98 ya maambukizo yote.

Ripoti ya shirika la afya duniani imeongeza kuwa, uwiano wa vifo barani Afrika uliongezeka kutoka asilimia 1.4 mwaka 2023 hadi asilimia 1.9 mwaka 2024.

Kipindupindu ni ugonjwa wa maambukizi ya utumbo mwembamba yanayosababishwa na bakteria, kinachoenea kwa kasi kupitia maji yaliyochafuliwa na kinyesi.

Mizozo, mabadiliko ya tabianchi, uhamaji wa watu, na uhaba wa muda mrefu wa miundombinu ya maji, ya udhibiti wa maji taka na usafi wa kiafya vinachochea kuongezeka kwa ugonjwa huo.

Takwimu za awali zinaonyesha kuwa janga la kipindupindu duniani linaendelea katika mwaka huu wa 2025, ambapo nchi na maeneo 31 yamekuwa yakiendelea kuripoti miripuko ya ugonjwa huo tangu mwanzoni mwa mwaka.../

Your Comment

You are replying to: .
captcha