15 Septemba 2025 - 23:39
Source: Parstoday
Araghchi: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iko bega kwa bega na Qatar na Waislamu wote

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ambaye yuko mjini Doha, Qatar kushiriki katika mkutano wa dharura wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi za Kiislamu na Kiarabu, amesisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu iko bega kwa bega na ndugu zake Waislamu wote.

Sayyid Abbas Araghchi, ameeleza hayo katika ujumbe alioweka kwenye mtandao wa kijamii wa X akisema: "niko mjini Doha nikiwa na ujumbe wa wazi kutoka kwa wananchi wa Iran: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iko bega kwa bega na Qatar; na kwa hakika, iko pamoja na ndugu zake Waislamu wote, hususan katika kukabiliana na janga linalotishia eneo zima".

Kikao cha pamoja cha Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC na wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kilianza jana Jumapili ya tarehe 13 Septemba huko Doha, mji mkuu wa Qatar kikihudhuriwa pia na Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Kikao hicho kinajadili uchokozi wa kijeshi uliofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Qatar.

Kikao hicho cha dharura cha Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Kiislamu na Kiarabu kimefanyika kwa ombi la Qatar ili kuzungumzia hujuma hizo za kijeshi zilizofanywa na utawala huo ghasibu dhidi ya ardhi yake.

Kikao hicho ni utangulizi wa mkutano wa viongozi wakuu wa nchi za Kiislamu na Kiarabu, ambao umepangwa kufanyika leo Jumatatu.

Rais Masoud Pezeshkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ni miongoni mwa viongozi wa nchi za Kiislamu za eneo watakaoshiriki katika mkutano huo.../

Your Comment

You are replying to: .
captcha