Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Ahlul-Bayt (AS) -ABNA- Ayatullah Isa Qassim, Mwanazuoni mashuhuri wa Bahrain, amesisitiza kuwa taifa huru na lenye heshima la Bahrain linataka kuachiliwa kwa watoto wao wapenda uhuru na kurejeshewa uhuru wao ulioporwa kwa dhulma.
Amesema: “Madai haya hayajatokana na upole wa kuomba msamaha au unyonge, bali ni katika muktadha wa haki yao ya kimaumbile, kisheria, kibinadamu na kidini - haki ya kuwa na uhuru, heshima, na hadhi - bila kutegemea fadhila au upendeleo kutoka kwa yeyote.”
Ayatullah Qassim ameweka wazi kuwa: “Suala hili si ombi la kuomba kwa njia ya hisani ili kupewa uhuru, bali ni madai ya haki ya uhuru ambao umechukuliwa kwa dhulma na kucheleweshwa kwa miaka mingi. Uhuru ni neema ya Mwenyezi Mungu na ni heshima kubwa kwa mwanadamu, na hakuna mtu yeyote anayeruhusiwa kuupokonya kutoka kwa mwingine isipokuwa kwa hukumu iliyo wazi na ya haki ya sheria ya Mwenyezi Mungu.”
Ameongeza kuwa wafungwa wa Bahrain ni watu waliotiwa gerezani kwa sababu ya kudai haki, kupinga dhulma, na kushikamana na amri ya kuamrisha mema na kukataza maovu.
Mwanazuoni huyo wa Bahrain amesisitiza: “Jamii ambayo ndani yake kudai haki kunatoweka na harakati za kuamrisha mema na kukataza maovu zinanyamazishwa, ni jamii isiyo na heshima, usalama, wala utulivu.”
Ayatullah Isa Qassim pia amekumbusha kuwa harakati ya mageuzi nchini Bahrain tangu mwanzo wake hadi leo imekuwa ikisisitiza njia ya amani, ingawa majibu ya serikali yamekuwa ya ukatili, vurugu, uharibifu wa vitu vitakatifu, na kunyang’anya uhuru kwa kiwango kikubwa.
Your Comment