11 Desemba 2025 - 15:52
France 24: Sera la Laicité  (Utaifa usioegemea Dini) nchini Ufaransa yageuzwa kuwa chombo cha shinikizo la kisiasa dhidi ya Waislamu

Wataalamu: Sheria hizi zinalenga kundi moja tu - Waislamu Nicolas Cadène, ambaye ni mtaalamu maarufu wa sheria ya Ulaikishe na aliyewahi kuwa ripota wa Kituo cha Uangalizi wa Ulaikishe, ameiambia France 24 kwamba: “Mipango hii inawalenga Waislamu pekee, na inaonyesha kukubalika kwa ubaguzi wa wazi.”

Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Ripoti mpya ya kituo cha habari France 24 inaonyesha kuwa mipango mipya ya chama cha mrengo wa kulia nchini Ufaransa kinachoitwa Warepublikan (Les Républicains) imekiuka wazi sheria ya mwaka 1905 kuhusu Ulaikishe (Laïcité — kanuni ya kutenganisha dini na serikali) na inalenga moja kwa moja jamii ya Waislamu. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Ulaikishe — ambayo kihistoria ilikusudiwa kulinda uhuru wa kuabudu — sasa inatumika kama silaha ya kisiasa ya kuwakandamiza Waislamu nchini humo.

Mashinikizo mapya dhidi ya Waislamu nchini Ufaransa

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Warepublikan wamewasilisha katika Bunge la Kitaifa mswada wa:

  • Kupiga marufuku hijabu kwa wasichana walio chini ya miaka 16,

na wakati huohuo, maseneta wa chama hicho wamependekeza masharti mengine mapya, yakiwemo:

  • 1-Marufuku ya kufunga mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwa watoto walio chini ya miaka 16,
  • 2-Kuwazuia akina mama waliovaa hijabu kushiriki katika safari au matembezi ya shule,
  • 3-Kupiga marufuku hijabu kwa wanamichezo wanawake.

Hatua hizi zote zinakinzana na kanuni ya kwanza ya sheria ya 9 Desemba 1905, inayolinda uhuru wa kuonyesha imani ya kidini na kutekeleza ibada bila kubughudhiwa.

Wataalamu: Sheria hizi zinalenga kundi moja tu - Waislamu

Nicolas Cadène, ambaye ni mtaalamu maarufu wa sheria ya Ulaikishe na aliyewahi kuwa ripota wa Kituo cha Uangalizi wa Ulaikishe, ameiambia France 24 kwamba: “Mipango hii inawalenga Waislamu pekee, na inaonyesha kukubalika kwa ubaguzi wa wazi.”

Ameonya kuwa mwelekeo wa kuitumia Ulaikishe kama chombo cha siasa umeanza katika makundi ya kulia kali, na sasa unaenea hadi vyama vya wastani, na kufanya: “Ulaikishe ya kulinda uhuru ibadilike kuwa Ulaikishe ya kukandamiza.”

Barua ya wazi ya wanaharakati Waislamu

Wanaharakati kadhaa Waislamu nchini Ufaransa — akiwemo Najat Ben Ali, Baciro Camara, na Abdennour Benattia — wametuma barua ya wazi kwa Rais wa Seneti ya Ufaransa wakionya kwamba: “Kuna mradi wa makusudi unaolenga kuifanya jamii ya Waislamu kuwa shabaha ya kisiasa.”

Wamekosoa msururu wa sheria mpya zinazolenga kupunguza uhuru wa kidini na haki za msingi za Waislamu kama raia wa Ufaransa.

Kupaa kwa wazo la “Ulaikishe ya Kupigana” (Laïcité de combat)

France 24 inataja pia kuongezeka kwa kile kinachoitwa Ulaikishe ya Kupigana — mtazamo mkali unaotaka kukandamiza kabisa alama zote za kidini katika jamii — unaohusishwa na:

  • Caroline Fourest
  • Élisabeth Badinter
  • Raphaël Enthoven

Mtazamo huu uliwahi kupata ushawishi mkubwa katika serikali ya Rais Macron na kusababisha:

  • sheria ya “kupambana na kujitenga na Jamhuri,”
  • marufuku ya abaya mashuleni,
  • na matamshi ya wazi ya kupinga Uislamu kutoka kwa baadhi ya mawaziri.

Ongezeko la chuki dhidi ya Uislamu katika vyombo vya habari

Ripoti hiyo inaeleza wazi kwamba vyombo vya habari nchini Ufaransa vimeongezeka kwa kasi kutoa matamshi ya chuki dhidi ya Uislamu, hali ambayo kwa mujibu wa Cadène:

  • inawafanya Waislamu wahisi kutengwa,
  • inatoa nafasi kwa makundi yenye misimamo mikali,
  • inazidisha mgawanyiko wa kijamii na chuki.

Ameonya kuwa sera hizi: “Hazitazaa matokeo mazuri, bali zitazalisha hali ya kujitenga na kufifisha mshikamano wa kitaifa.”

Takwimu za kusikitisha: 82% ya Waislamu wanahisi chuki imeenea

Kulingana na utafiti wa taasisi ya uchunguzi wa maoni IFOP, kwa ombi la Msikiti Mkuu wa Paris, takwimu zinaonyesha kuwa:

  • 82% ya Waislamu nchini Ufaransa wanaamini kuwa chuki dhidi yao ni “pana na inayoonekana wazi,”
  • 81% wanaamini kuwa hali imezidi kuwa mbaya zaidi katika miaka 10 iliyopita.

Kwa mujibu wa wachambuzi, hii inaonyesha kuongezeka kwa: “Islamophobia ya kiserikali na ya kimfumo”

chini ya mwamvuli wa “kulinda maadili ya Jamhuri,” lakini kivitendo ikitumiwa kama zana ya kuwakandamiza Waislamu nchini humo.

Tags

Your Comment

You are replying to: .
captcha