Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Katika mazingira ya kuimarisha uelewano na mshikamano wa kidini, wanazuoni wa Kikristo na Kiislamu nchini Malawi wamekutana katika mjadala wa kielimu uliolenga kuangazia dhana ya Mkombozi wa Ulimwengu kwa mujibu wa mafundisho ya dini zao, ukiwa ni mjadala ulioandaliwa na Kuratibiwa na Uwakilishi wa Jamiatul Mustafa (s) International Foundation, Tawi la Malawi, chini ya Uongozi wa Hujjatul-Islam Wal-Muslimin Dr.Ali Taqavi.
Katika mjadala huo wa kielimu, kila upande uliwasilisha mtazamo wake kuhusu Kiongozi na Muokozi au Mkombozi anayengojewa katika zama za mwisho - na huyo ni kiongozi ambaye atakuja kuleta haki, amani na uadilifu katika dunia iliyogubikwa na migogoro, dhulma na maovu ya kijamii.
Kwa upande wa Kikristo, washiriki waliowakilisha Imani ya Dini ya kikristo, walieleza imani ya kungojea kurejea kwa Yesu Kristo kama Mwokozi wa wanadamu, atakayekuja kuimarisha ufalme wa haki na kuleta wokovu kwa waumini.
Kwa upande wa Kiislamu, Wanazuoni walifafanua itikadi ya kumngojea kudhihiri kwa Imam Mahdi (atfs), ambaye kwa mujibu wa mafundisho ya Kiislamu atadhihiri kwa amri ya Mwenyezi Mungu katika wakati uliopangwa, ili kuujaza ulimwengu kwa haki na uadilifu kama ulivyojaa dhulma na uonevu. Aidha, ilielezwa kuwa kudhihiri kwake kutakuwa sehemu ya mpango wa kimungu wa kurejesha mizani ya maadili na kusimamisha uongozi wa haki.
Washiriki wa mjadala walisisitiza kuwa licha ya tofauti za kiteolojia, dini zote zinashirikiana katika tumaini la pamoja la kuja kwa zama za haki na amani. Dhana ya Mkombozi imeonekana kuwa daraja la mazungumzo ya kidini linaloweza kuimarisha uelewano, kuheshimiana na mshikamano miongoni mwa waumini wa dini tofauti.
Mjadala huo ulihitimishwa kwa wito wa kuendeleza mazungumzo ya kielimu na kushirikiana katika kujenga jamii inayozingatia maadili, haki na utu wa mwanadamu, huku kila dini ikiendelea kuheshimu misingi na itikadi zake.
Your Comment