Mustafa Abduljalil, mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Mpito NTC jana alitoa matamshi ya kuunga mkono kuendelea kuwepo nchini humo vikosi vya NATO na akasema, NATO inapasa kuendelea kubaki nchini Libya hadi mwishoni mwa mwaka huu wa 2011. Kwa mujibu wa Abduljalil kuwazuia waungaji mkono wa utawala wa zamani wa Libya wasiweze kutoroka ndicho kipaumbele cha kwanza cha Baraza la Taifa la Mpito; na kwamba ili kuweza kufikiwa lengo hilo kuna ulazima wa operesheni za kijeshi na NATO kuendelea kufanywa nchini humo. Hii ni katika hali ambayo kamanda wa NATO nchini Libya amesema vikosi vya NTC vinao uwezo wa kulinda usalama wa nchi yao. Wakati huohuo baraza la kijeshi la mji wa Misrata ulioko kaskazini magharibi mwa Libya limetangaza kuwa brigedi ya "Ngome Nyekundu" ya mji huo imevunjwa, na silaha za wapiganaji wa brigedi hiyo zimekabidhiwa kwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Libya. Kwa mujibu wa baraza hilo brigedi ya "Ngome Nyekundu" ilikuwa na wapiganaji 600 ambao walishiriki katika mapambano ya kuukomboa mji mkuu Tripoli na ule wa Sirte.Ripoti nyengine kutoka Libya zinaeleza kuwa maiti za watu 267 ambao wengi wao walifariki kwa kunyongwa zimegunduliwa katika mji wa Sirte. Shirika la kutetea haki za binadamu limetangaza kuwa siku ya Jumatatu iliyopita liligundua viwiliwili 53 vya wafuasi wa Gaddafi ndani ya hoteli moja mjini Sirte.Mbali na nafasi ya Baraza la Taifa la Mpito na shirika la kijeshi la NATO, familia ya Muammar Gaddafi ni mhimili mwengine wa tatu wa matukio ya Libya. Marcel Ceccaldi ambaye ni wakili wa familia ya Gaddafi amesema familia hiyo inakusudia kufungua mashtaka dhidi ya NATO ya kuhusika na mauaji ya Muammar Gaddafi. Kwa mujibu wa Ceccaldi familia hiyo imekusudia kufungua mashtaka katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC dhidi ya NATO ya kutenda jinai za kivita katika mauaji ya Gaddafi. Wakili wa familia ya Gaddafi amesema ndege za vikosi vya NATO ziliishambulia gari iliyokuwa imembeba Gaddafi katika mji wa Sirte ambayo haikuwa ni tishio kwa raia. Wakati huohuo Saiful Islam, mwana wa dikteta wa Libya ambaye inavyoonekana alinusurika katika kizaazaa cha vita na mashambulio yaliyohatimisha maisha ya baba yake amesikika katika ujumbe aliotoa hivi karibuni akitoa vitisho kwa shirika la kijeshi la NATO na kwa vikosi vya wanamapinduzi kwamba mto wa damu utashuhudiwa ndani ya Libya. Aidha amesema ataahirisha kuweka matanga ya baba yake na ndugu yake mpaka atakapokamilisha kazi yake hata kama suala hilo litachukua muda wa miaka 50. Mwana huyo wa Gaddafi ambaye inaaminika kuwa hivi sasa yuko kaskazini mwa Niger amedai pia kwamba kuna watu wengi sana wanaoomboleza pamoja naye kifo cha baba yake na ambao wako tayari kwa mapambano ili kulipiza kisasi kwa wauaji wa Gaddafi.
19 Machi 2011 - 20:30
Msimbo wa Habari: 275013
Kwa kuuawa dikteta wa Libya Muammar Gaddafi, awamu mpya ya matukio imeanza nchini humo chini ya mihilimi mitatu ya Wanamapinduzi, shirika la kijeshi la NATO na familia ya Gaddafi