Ali Abdullah Saleh ni dikteta aliyewafutilia mbali wapinzani wake wote katika masuala ya siasa mmoja baada ya mwingine na kuweza kuitawala Yemen kwa ngumi ya chuma kwa kipindi cha miaka 33. Dikteta huyo pia alikuwa na nia kuufanya mfumo wa uongozi wa nchi hiyo kuwa wa kifamilia kupitia njia ya kumrithisha madaraka mwanaye. Hata hivyo ndoto na matarajio yote ya dikteta huyo yamesambaratika baada ya kuanza harakati za mapinduzi ya wananchi wa Yemen, jambo lililozidisha hasira na munkari wa Abdullah Saleh.
Mashambulizi yaliyofanywa na wanamapinduzi wa Yemen miezi mitatu iliyopita katika ikulu ya Rais na kumjeruhi Saleh yamezididha mara dufu chuki zake dhidi ya wananchi wanaofanya maandamano na wapinzani wake.
Hivi sasa ambapo kuna mjadala wa kukabidhi madaraka ya nchi kwa makamu wa rais wa Yemen kwa mujibu wa mpango uliopendekezwa na Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi, inaonekana kuwa Saleh anajaribu kila awezalo kupoteza wakati, huku akiendelea kuzusha hali ya hofu na wasiwasi nchini humo ili kuandaa mazingira mazuri ya kuwatwisha wananchi matakwa yake katika utekelezaji wa mpango huo. Hasa ikizingatiwa kuwa ujumbe wa wapinzani wa Yemen unatazamia kuelekea mjini Riyadh, Saudi Arabia kwa majadiliano zaidi. Saleh anajaribu kutumia njia zote zinazowekana ili apewe kinga ya kutoshtakiwa yeye pamoja na familia yake. Kwa msingi huo ameshurutisha kwamba atasaini mkataba huo iwapo tu matakwa hayo yatazingatiwa.
Wakati huo huo wananchi wa Yemen wanamtambua Ali Abdullah Swaleh kuwa ni dikteta mtenda jinai ambaye mikono yake imejaa damu za raia wasiokuwa na hatia na wanasisitiza juu ya udharura wa kufikishwa mahakamani dikteta huyo. Wananchi wa Yemen wanapinga mapatano yoyote yatakayopelekea kupewa kinga ya kisheria dikteta huyo, suala ambalo litakuwa changamoto kubwa kwa ujumbe wa Yemen ulioelekea Riyadh kwa ajili ya kutafuta ufumbuzi wa mgogoro wa sasa wa nchi hiyo.
19 Machi 2011 - 20:30
Msimbo wa Habari: 277925
Maandamano ya Ijumaa ya jana huko Yemen hususan katika mji wa Taiz yaligubikwa na umwagaji damu mkubwa. Baadhi ya duru za habari zimeitaja idadi ya waliouawa na kujeruhiwa huko Yemen kuwa ni zaidi ya watu mia moja. Miongoni mwa jinai zilizofanywa jana na utawala wa Rais Ali Abdallah Saleh ni kushambulia hospitali iliyokuwa imefurika wagonjwa huko kusini mwa Yemen na kuua raia waliokuwa wakisali. Katika siku za hivi karibuni dikteta Abdullah Saleh amekuwa akiwatumia kikosi maalumu cha Gadi ya Ulinzi wa Rais kuwashambulia waandamanaji wanaopinga utawala wake.